Home » » RC AWAONYA MADIWANI

RC AWAONYA MADIWANI

na Samwel Mwanga, Simiyu
SERIKALI mkoani Simiyu imeonya tabia ya baadhi ya madiwani kuingilia shughuli na utendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), badala yake iheshimiwe na kupewa ushirikiano kwani haina mipaka katika utendaji wake kazi hasa katika masuala ya uchunguzi.
Onyo hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Mkoa (RC), Paschal Mabiti, alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Wilaya ya Meatu baada ya ziara ya siku mbili wilayani hapa na kujibu hoja ya madiwani kumkataa Ofisa wa TAKUKURU Wilaya ya Meatu, Damas Sutta.
Mabiti alikuwa akijibu hoja zilizotolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Pius Machungwa alipohoji hatua zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya ofisa huyo anayedaiwa kuwatishia viongozi na watumishi na kufanya kazi zake kinyume na utaratibu.
Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, wiki iliyopita lilimkataa ofisa huyo kwa madai ya kumhoji mfanyakazi wa Idara ya Kilimo na Mifugo, Jesca Shadrack kwa tuhuma za rushwa.
Mbali ya kumkataa ofisa huyo, pia madiwani walieleza masikitiko yao kutokana na tukio la ofisa huyo kumhoji mfanyakazi huyo hadi akaanguka na kupoteza fahamu.
Awali, Machungwa alisema kutokana na kuchoshwa na vitendo vya ofisa huyo, wanaiomba serikali ifanye utaratibu wa kumhamisha.
Kwa upande wake, ofisa huyo wa TAKUKURU alikiri kumuhoji Shadrack ambaye anatuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha za halmashauri kiasi cha sh milioni tano zilizotolewa kwa ajili ya kuendeshea shughuli za mashamba darasa na kwamba wakiwa katika mahojiano ghafla alianguka na kupoteza fahamu.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa