Na Christopher Gamaina, Busega
WAKAZI wa kijiji cha Lukungu katika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, wanatarajiwa kunufaika na huduma bora za afya, kufuatia ukarabati wa zahanati ya kijiji hicho utakaogharimiwa na taasisi ya Serikali ya Utafiti wa Dawa (MR) tawi la Mwanza.
Ukarabati wa zahanati hiyo utawaondolea wakazi wa kijiji hicho adha ya kusafiri umbali mrefu kwenda kutafuta huduma za afya katika wilaya za Bunda mkoani Mara na Magu mkoani Mwanza.
Dk. Safari Kinungi kutoka MR Mwanza, ameahidi kwamba ofisi yake itakuwa tayari kugharimia ukarabati wa zahanati hiyo baada ya kutayarishiwa tathmini ya mahitaji na gharama husika.
Kwa mujibu wa Dk. Kinungi, ofisi yake imeridhia kugharimia ukarabati wa zahanati hiyo baada ya kuombwa na Mbunge wa Jimbo la Busega, Dk. Titus Kamani (CCM).
Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Lamadi kilipo kijiji cha Lukungu, Bw. Emmanuel Desela, amesema tayari Halmashauri ya Wilaya ya Busega imeshaidhinisha Sh milioni 16.2 kuchangia gharama za ukarabati wa zahanati hiyo.
Watumishi wa zahanati hiyo, Dk. Erick Samwel na Muuguzi Ester Biyila, wametaja baadhi ya matatizo yaliyopo kuwa ni uchakavu wa majengo, ukosefu wa maji, maabara, umeme, gari la wagonjwa, upungufu wa vitendea kazi, watumishi na vyoo.
Pamoja na majukumu mengine, taasisi ya MR Mwanza inatekeleza mradi wa kupima na kutibu magonjwa ya kichocho na minyoo ya tumbo shuleni.
0 comments:
Post a Comment