na Samwel Mwanga, Simiyu
HALMASHAURI saba zinazostawisha Pamba katika mikoa ya Simiyu na Shinyanga zimeonana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuzungumzia agizo la serikali kuridhia kushushwa kwa ushuru wa zao hilo kutoka asilimia tano hadi mbili unaokusanywa na halmashauri.
Aidha mazungumzo hayo yalilenga kuiomba serikali kunusuru bei ya pamba msimu huu badala yake izipatie fidia juu ya kutotoza ushuru huo msimu huu. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT) Mkoa wa Shinyanga Pius Machungwa akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi jana alisema hatua hiyo imefikiwa ili serikali iangalie.
upya agizo lake kuridhia kushushwa kwa ushuru wa zao hilo. Halmashauri zilizofanikiwa kuonana na waziri mkuu ni Meatu, Bariadi, Maswa, Kishapu, Shinyanga Manispaa, Kahama na Bukombe ambazo zimedai kuathiriwa na agizo hilo. Machungwa alisema ujumbe huo wa wenyeviti wa halmashauri hizo umekutana na waziri mkuu juzi na kuiomba serikali iangalie uwezekano wa kufidia fedha na kuziba pengo la asilimia tatu katika msimu wa ununuzi wa za hilo mwaka huu na kufikia asilimia tano ya awali kama ilivyo kuwa misimu iliyopita.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Meatu alisema lengo la halmashauri hizo ni kuiomba serikali kukubali kuzilipa fidia ya asilimia tatu halmashauri hizo ili zitekeleze miradi yake ya maendeleo na miundombinu kwa mujibu wa bajeti iliyokuwepo kabla ya kuathiriwa na mdororo wa bei ya zao hilo katika soko la dunia.
Alisema athari kubwa ni kwa halmashauri hizo kushindwa kuchangia katika miradi ya maendeleo ya mwaka 2012/13 kama ilivyopangwa katika bajeti za halmashauri hizo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment