na Samwel Mwanga, Maswa-Simiyu
RAIS Jakaya Kikwete ametakiwa kutoa kauli juu ya bei ya zao pamba ambayo imeleta mtafaruku mkubwa kati ya wakulima na wanunuzi wa zao hilo.
Mtafaruku huo umesababisha amani kutoweka kutokana na wakulima kuwashambulia na kuwajeruhi wanunuzi wa zao hilo wanaonunua kwa bei ya sh 640 kwa kilo.
Kauli hiyo ilitolewa na Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (CHADEMA) alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo.
Alisema zao la pamba limekuwa halipewi kipaumbele na serikali, hivyo mkulima amebaki akitangatanga huku asijue la kufanya kutokana na bei yake kuyumbayumba kila mwaka.
“Mkulima wa pamba amekuwa hapewi kipaumbele na serikali, kwani kwa sasa bei haijulikani ni ipi na wanunuzi wanataka kununua kwa sh 640 kwa kilo badala ya sh. 1,000 kama ilivyotamkwa na wawakilishi wao bungeni, ” alisema.
“Wakati wa utawala wa TANU ambapo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliongoza kulikuwepo na Victoria Federation hii ilikuwa mahususi kwa ajili ya kusimamia zao la pamba na hivyo hakukuwa na malamiko kama yaliyo sasa,” alisema.
Alisema ukimya wa serikali juu ya kauli zilizotolewa bungeni na baadhi ya wawakilishi wa wananchi wanaotoka maeneo yanayolimwa pamba kuwa hakuna kuuza kilo moja chini ya sh 1,000 ndio umeifikisha nchi katika hatua hiyo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment