na Samwel Mwanga, Maswa
IDARA ya Elimu wilayani hapa mkoani Simiyu, imetangaza utaratibu wa kuwapima ujauzito wanafunzi wa kike wa kuanzia darasa la tatu hadi la saba, kwa lengo la kudhibiti vitendo vilivyokithiri vya wanafunzi hao kupata ujauzito.
Uamuzi huo ambao utekelezaji wake utaanza mwezi ujao, ulifikiwa jana katika kikao cha wadau wa elimu wilayani hapa kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, ili kujadili na kutathmini changamoto zinazoikabili Idara ya Elimu katika kipindi cha mwaka 2009 hadi 2011 na kusababisha kupungua kwa kiwango cha taaluma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Madiwani ya Elimu, Afya na Maji, Raphael Kudomya ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Dakama, alisema moja ya matatizo makubwa yanayosababisha kushuka kwa kiwango cha elimu wilayani hapa ni pamoja na wanafunzi wa kike kupatiwa ujauzito wakiwa shuleni.
“Katika wilaya yetu tuna tatizo kubwa la wanafunzi wetu wa kike hasa wa shule za msingi kutomaliza masomo yao kwa kupatiwa ujauzito, suala hili linachangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa kiwango cha elimu,” alisema.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Mhandisi Nicholaus Francis alisema hatua iliyofikiwa na wadau ina lengo la kudhibiti vitendo vya ngono kwa wanafunzi walioko katika madarasa hayo kwani wengi wao ni wenye umri wa kati ya miaka minane hadi 16.
Aliongeza kuwa, zoezi hilo litakuwa kila baada ya miezi mitatu kwa kuwatumia wataalamu wa idara ya afya wa wilaya hiyo.
Takwimu zinaonesha katika kipindi cha mwaka mmoja, zaidi ya wanafunzi 50 wa kike wa shule za msingi wilayani hapa wamelazimika kuacha masomo kutokana na kupata ujauzito
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment