na Samwel Mwanga, Maswa
MAPAMBANO makali yamezuka kati ya askari polisi na wananchi katika mji wa Malampaka, wilayani hapa kutokana na askari mgambo, Abdallah Ally kumpa kipigo, dereva wa pikipiki, Malando Masele.
Watu walioshuhudia tukio hilo waliliambia Tanzania Daima kuwa, tukio hilo lilitokea juzi, majira ya saa 10:30 jioni na kusababisha baadhi ya watu kujeruhiwa na shughuli nyingi za kijamii kusimama kwa takribani saa tano.
Walisema askari huyo alimkamata Masele akiendesha pikipiki bila kuvaa kofia ngumu (Helmet), hivyo kumwamuru aende kituo cha polisi, lakini alikataa na ndipo alianza kumshambulia kwa kumpiga kwa kutumia nondo aliyokuwa nayo na kisha kukimbilia Kituo cha Polisi Malampaka.
“Chanzo cha vurugu hizi zote zilizotokea ni baada ya huyu mgambo kumkamata Masele akiwa anaendesha pikipiki yake bila kuvaa helmet na hivyo kumwamuru aende kituoni, lakini alikataa na ndipo alipoanza kumshambulia Masele,” alisema Juma Said.
Walisema kuwa baada ya askari huyo kukimbilia kituoni, vijana wapatao 20 walikivamia kituo hicho huku wakiwa na mwenzao aliyepigwa na kutaka apatiwe fomu ya matibabu (PF 3) ili akatibiwe, lakini alikataa ndipo walianza kukishambulia kituo hicho cha polisi kwa mawe na kutishia kukichoma moto.
Kutokana na hali hiyo, askari aliyekuwapo kituoni hapo alipiga risasi hewani, lakini wananchi walizidi kuongezeka na kuendelea kukishambulia kituo hicho na ndipo askari Ally akapata mwanya na kukimbilia nyumbani kwao, lakini walimfuata na kuishambulia kwa kuibomoa hadi walipotawanywa na mabomu ya machozi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Salum Msangi alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema polisi inafanya uchunguzi na wahusika wote watakaobainika kuwa chanzo cha vurugu hizo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Chanzo: Tanzania Diama
0 comments:
Post a Comment