Home » » Harambee ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi wilayani Bariadi

Harambee ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi wilayani Bariadi

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

 Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), Ndg.Mark Malekana akizungumza na  wananchi wa Gambosi(hawapo pichani)  wakati wa  Harambee ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi iliyofanyika jana katika kijiji cha Gambosi wilayani Bariadi.
 Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), Ndg.Mark Malekana (kushoto) Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (kulia) wakisaini vitabu vya wageni wakati wa  Harambee ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi, iliyofanyika jana katika kijiji cha Gambosi wilayani Bariadi.
 Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akizungumza na wananchi wa Gambosi (hawapo pichani) wakati wa  Harambee ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi iliyofanyika jana katika kijiji cha Gambosi wilayani Bariadi.
 Kutoka kulia Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) wakiwa na viongozi wengine wakati walipotembelea eneo la ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi kabla ya kufanya harambee ya ujenzi wa shule hiyo kijijini Gambosi (Bariadi).
 Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Gambosi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) wakati wa  Harambee ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi iliyofanyika jana kijijini hapo wilayani Bariadi.
 Diwani wa Kata ya Gambosi, Mhe.Bahame Kaliwa akizungumza na wananchi wa Gambosi (hawapo pichani)  wakati wa  Harambee ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi iliyofanyika jana katika kijiji cha Gambosi wilayani Bariadi.
 Paroko wa Parokia ya Ngulyati wilayani Bariadi akizungumza na wananchi wa Gambosi (hawapo pichani) wakati wa  Harambee ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi iliyofanyika jana katika kijiji cha Gambosi wilayani Bariadi.
 Mbunge wa Jimbo la Itilima ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Mkoa wa Simiyu, Mhe.Njalu Silanga akizungumza na wananchi wa Gambosi (hawapo pichani) kabla ya kuchangia katika  Harambee ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi iliyofanyika jana katika kijiji cha Gambosi wilayani Bariadi.
 Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Mhe.Duka Mashaurimapya akipeana mkono na Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), Ndg.Mark Malekana baada ya kuwasilisha mchango wa Halmashauri hiyo wakati wa  Harambee ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi iliyofanyika jana katika kijiji cha Gambosi.
 Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Simiyu na Mbunge wa Itilima ,akipeana mkono na Diwani wa Kata ya Gambosi Mhe. Bahame Kaliwa, baada ya kuwasilisha mchango wake wakati wa  Harambee ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi iliyofanyika jana katika kijiji cha Gambosi.
 Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), Ndg.Mark Malekana akimuonesha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka  risiti aliyopewa baada ya kununua mifuko 100 ya saruji  kwa ajili ya  kuchangia Ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi.
 Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Gambosi wakienda kuchangia wakati wa Harambee ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi iliyofanyika jana katika kijijini hapo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (kulia) akizungumza na wananchi wa Gambosi (hawapo pichani) wakati wa  Harambee ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi iliyofanyika jana katika kijiji cha Gambosi wilayani Bariadi




Na Stella Kalinga

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka ameongoza harambee ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Gambosi iliyopo Kata ya Gambosi wilayani Bariadi Mkoani humo.

Harambee hiyo imefanyika kufuatia azma ya Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Tanzania, Ndg.Mark Malekana kutaka kuunga mkono juhudi za wananchi wa kata aliyozaliwa ya Gambosi katika ujenzi wa shule hiyo, kwa kuwa watoto wa kata hiyo wamekuwa wakisoma katika shule ya sekondari Miswaki kata ya jirani ya Mwasubuya.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi, Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Gambosi, Longino Nasari amesema Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi kwa kushirikiana na wananchi wameanza kwa kujenga vyumba vitatu vya maabara, jengo la utawala na matundu 08 ya vyoo.

Askofu Malekana amewataka wananchi wa Gambosi kushirikiana na Serikali kujenga shule na miundombinu mingine ya Huduma za Jamii bila kujali tofauti zao za kiitikadi na dini ili kuitengeneza Gambosi mpya ya tofauti na jinsi inavyodhaniwa na watu kuwa ni mahali penye mambo ya kishirikina.

Aidha, Askofu Malekana ametoa wito kwa wananchi wa Gambosi hususani vijana kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo katika eneo hilo na kubadili fikra na mtazamo wa watu wengi juu ya eneo hilo.

“Maendeleo hayaji kwa muujiza wala hayaji kwa bahati mbaya, acheni hadithi za kusema kama Mungu kakupangia kufa maskini utakufa maskini, au kama ulipangiwa kuwa na tajiri utakuwa hivyo, hapana Mungu hakupanga hivyo. Muachane kabisa na fikra hizo potofu fanyeni kazi kwa bidii, mjenge Gambosi Mpya”

Pamoja na kuhimiza maendeleo Askofu Malekana amewataka wananchi wa Gambosi kudumisha amani na kuwatengenezea mazingira rafiki watumishi wanaopangwa kufanya kazi katika eneo  hilo ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za kupangisha ili waone fahari kufanya kazi Gambosi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amewataka wananchi kuona umuhimu wa elimu na kuwapeleka shule watoto wote wanaopaswa kwenda shule mapema mwezi Januari, 2017 shule zitakapofunguliwa.

Wakati huo huo Mtaka amewataka wananchi kuvitumia vituo vya kutolea huduma za Afya pale wanapougua badala ya kwenda kwa waganga wa jadi ili kupunguza vifo visivyo vya lazima vinaivyoibua chuki  na visasi vitokanavyo na ramli chonganishi, ikiwa ni pamoja na ukataji wa mapanga kwa vikongwe kwa imani za kishirikina.

“Tumieni vituo vyetu vya huduma za Afya vilivyopo  ili mfanyiwe uchunguzi na kupewa tiba kwa gharama nafuu; wazee na watoto chini ya miaka mitano wanatibiwa bure. Pamoja na unafuu huo unasikia mtu anampeleka mtoto kwa mganga anachanjwa chale akifikishwa hospitali hana damu hana maji anakufa, akifa mnaanza kutafuta mchawi, hiyo tabia iachwe kabisa” amesema Mtaka

Katika Harambee hiyo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi mifuko 604 ya saruji, nondo 100, bati 20, misumari kilogramu 7, Madawati 80, Unga wa Ngano mfuko mmoja na mafuta ya kula katoni 1 kwa ajili ya chakula cha mafundi, vitabu 18 na fedha taslimu vilipatikana, vyote vikiwa na thamani ya shilingi 21,761,050, ikiwa ni michango ya Askofu wa Kanisa la SDA Tanzania na wadau wake, Viongozi wa Serikali ya Mkoa na Wilaya, Wafanyabiashara wa Bariadi na wananchi wa Gambosi.

Mkuu wa Mkoa amehimiza fedha hizo zitumike kwa makusudi yaliyokusudiwa na ujenzi uendelee ili kufikia mwaka 2018 shule hiyo ifunguliwe.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa