Na. Mwandishi Wetu
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya
Watu wenye Ulemavu, Mhe. Dkt. Abdallah Possi amezitaka
Halmashauri zote nchini kutekeleza agizo la kuunda Kamati za Watu Wenye Ulemavu kuanzi
ngazi ya Vijiji, Kata, Wilaya hadi Mkoa.
Mhe. Possi ametoa maagizo hayo kwa nyakati tofauti wakati wa
ziara yake katika mikoa ya Mwanza na Simiyu hivi karibuni ambapo
alitembelea makazi
ya watu wenye mahitaji maalum ya Bukumbi, Shule ya watu wenye mahitaji
maalum ya Mitindo na kituo cha kulelea watoto wenye ualbino cha Lamadi.
Kauli ya Dkt. Possi imekuja kufuatia maagizo yaliyolewa
na Ofisi ya Waziri Mkuu mwezi Machi mwaka huu kwa kuziandikia Halmashauri
zote kutekeleza uundwaji wa kamati za Watu wenye Ulemavu ikiwa ni sehemu ya kutatua changamoto wanazokabiliana nazo.
“Ni muhimu sana kutekeleza agizo lililotolewa na
Ofisi ya Waziri Mkuu mwanzoni mwa mwaka huu ambalo limeeleza wazi kuundwa kwa
Kamati za Watu wenye Ulemavu na ikumbukwe kuwa, suala hii lipo kisheria na lina
miongozo yake katika utekelezaji wake”. Alisema Waziri Possi.
Waziri Possi alisisitiza kuwa maagizo ya kuundwa kwa kamati
za watu wenye ulemavu yalitolewa na Ofisi hiyo ili kusaidia upatikanaji
sahihi wa taarifa za watu wenye ulemavu ili kupata namna bora ya kutatua
changamoto zinazowakabili.
“Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa agizo hilo ili
kusaidia kujua mahitaji ya watu wenye ulemavu na kuwa na njia nzuri za utatuzi
wa changamoto zao kwa kuzingatia takwimu sahihi zitakazo toa picha halisi ya
hali zao katika nyanja zote.”Alisema Dkt.Possi
Aliongeza kuwa
Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kutoa vipaumbele kwa watu wenye
ulemavu na mahitaji maalum kwa kuwapa nafasi za ushiriki katika mipango yote ya maendeleo ikiwemo;
elimu, huduma za afya na uchumi ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha katika jamii.
Nae Mkuu
wa Wilaya ya Misungwi Mhe. Juma Sweda alimpongeza Mhe. Possi kwa
juhudi za kuhakikisha sauti za watu wenye ulemavu
zinasikika katika ngazi zote kwa kuudwa kwa kamati hizo zitazotatua na kutibu
changamoto za watu wenye ulemavu.
”Nikupongeze Mhe. Waziri kwa kutembelea Wilaya yetu na kuona
umuhimu wa kuweka msisitizo wa uundwaji wa Kamati hizi, nasi tunakuhaidi
kulitekeleza hilo kama Ofisi yako ilivyoekeza ili kufikia malengo ya Serikali
katika kuhakikisha Haki na Usawa unakuwepo kwa watu wote bila kujali hali
zao”.Alisema Mhe.Sweda.
0 comments:
Post a Comment