Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony J. Mtaka
akizungumza na waandishi wa habari juu ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru,
Kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa na Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Oktoba 14
mwaka 2016, yatakayofanyika mkoani humo.
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony J. Mtaka akizungumza na waandishi wa habari juu
ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa na
Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Oktoba 14 mwaka 2016, yatakayofanyika mkoani humo.
Baadhi
ya vijana wa Wilaya ya Maswa wakiwa katika zoezi la uzalishaji chaki katika
kiwanda cha kutengeneza chaki kilichopo wilayani humo ambacho kinazalisha chaki
zinazotambulika sokoni kama Mzinazotumika mkoani Simiyu.
Baadhi
ya vijana wa Wilaya ya Meatu wakielekezwa namna ya kupima maziwa na kutambua
maziwa bora yasiyo na maji, katika kiwanda chao cha uzalishaji wa maziwa
yanayotambulika sokoni kama ‘MEATU MILK’
Sehemu ya Jengo la Ofisi ya Vijana wa Wilaya ya Meatu
wanaojishughulisha na usindikaji wa maziwa (MEATU MILK).
Na
Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa
wito kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu na Taifa kwa ujumla kushiriki katika Kilele
cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa na
Maadhimisho ya Wiki ya Vijana mwaka 2016, yatakayofanyika mkoani humo.
Akizungumza na waandishi wa Habari Ofisini kwake Mtaka
amesema Mkoa wa Simiyu umepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa Kilele cha Mbio za Mwenge
wa Uhuru, Kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa na Maadhimisho ya Wiki ya Vijana
yatakayofanyika Oktoba 14, 2016 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Mtaka ameeleza kuwa Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
ambaye pia atashiriki Ibada ya
Kumbukumbu ya Kifo cha Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere,
itakayofanyika siku hiyo ya tarehe 14 Oktoba, 2016 katika Kanisa Katoliki la
Mtakatifu Yohana, Mjini Bariadi kuanzia saa 1:00 kamili asubuhi.
Wakati huo huo Mtaka amesema maadhimisho ya wiki ya vijana
yatafunguliwa rasmi tarehe 08 Oktoba, 2016 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama
(Mb) katika Uwanja wa SABASABA Mjini Bariadi; ambapo shughuli mbalimbali za
vikundi vya maendeleo ya vijana kutoka Halmashauri zote nchini zikiwemo za
ujasiriamali pamoja na ugunduzi wa kisayansi ambao umethibitishwa na Tume ya
Taifa ya Sayansi zitaoneshwa katika mabanda maalum yaliyojengwa katika uwanja huo.
“Kwa upande
mkoa wa Simiyu vikundi vyetu vya vijana vimejiandaa kuonesha shughuli
mbalimbali za kiuchumi zinazofanywa katika Halmashauri husika;ambapo kimkoa
tunatekeleza mkakati wa kila wilaya kuzalisha bidhaa/huduma moja yaani (one
district one product).
Kulingana na mkakati huo Vijana wa Wilaya ya
Meatu wameanzisha kiwanda cha kusindika maziwa ya ng’ombe, Maswa kiwanda cha
kuzalisha chaki na wilaya nyingine tunaendelea kujipanga kuzalisha bidhaa
nyingine” alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka amewakumbusha wananchi wa Mkoa wa
Simiyu kuwa Maadhimisho haya ni fursa kwao kiuchumi na kijamii kwa kuwa
watapokea wageni wengi kutoka maeneo mbalimbali nchini ambao watahitaji malazi,
chakula na huduma nyingine muhimu, hivyo waoneshe ukarimu na ushirikiano wa
hali ya juu ili kuupa heshima mkoa huo.
Naye Pendo Benjamin Mkazi wa Mtaa wa Sima mjini
Bariadi amesema amepokea kwa furaha suala la kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru
kufanyika mkoani Simiyu kwa kuwa ni la kihistoria, pia ni fursa kwa wafanyabiashara
wa vyakula, nyumba za kulala wageni na mahitaji mengine.
Sanjali na hilo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ametoa wito
kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kuchangia damu kwa hiari katika uwanja wa
SABASABA kuanzia tarehe 08/10/2016 hadi 13/10/2016, zoezi ambalo litafanywa na Hospitali
Teule ya Rufaa ya Mkoa kwa kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu na
Shirika la AGPAHI kwa ajili ya
kuwasaidia watu wenye uhitaji wa damu hususani mama wajawazito, majeruhi wa
ajali na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya
kifo cha Baba wa Taifa na Maadhimisho ya Wiki ya Vijana kwa mwaka 2016 ni tukio
la kihistoria kwa Mkoa wa Simiyu na la kwanza kwa Mhe.Rais wa awamu ya tano
tangu alipopata ridhaa ya wananchi kuliongoza Taifa letu.
0 comments:
Post a Comment