Home » » KINA CHENGE, TIBAIJUKA KULA KIBANO ESCROW LEO.

KINA CHENGE, TIBAIJUKA KULA KIBANO ESCROW LEO.

  Uchunguzi dhidi ya �majaji washika kasi.
Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.
 
Wiki hii inatarajiwa kuwa ngumu kwa wanufaika wa mgawo wa uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow, wakati Baraza la Maadili litakapowaweka kikaangoni watuhumiwa kadhaa, wakiwamo, Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.
 
Kwa mujibu wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Baraza la Maadili, litaanza vikao vya kuwahoji watuhumiwa mbalimbali kwa wiki tatu mfululizo jijini Dar es Salaam kuanzia leo.
 
Watuhumiwa wengine wa Escrow ambao watawekwa kitimoto ni aliyekuwa Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa.
 
Wabunge hao ni miongoni mwa vigogo tisa wanaotuhumiwa kunufaika na fedha hizo na watafika mbele ya baraza hilo. Kwa mujibu wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa  Umma, watuhumiwa wengine wawili ni Meya wa Manispaa ya Tabora na aliyekuwa Mkuu Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo.
 
Baraza hilo litatoa uamuzi wa ama wahusika hao kufikishwa mahakamani au la, kulingana na hatia watakazokutwa nazo.
 
 Akizungumza na NIPASHE jana, Ofisa Habari wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Johanither Barongo, alithibitisha kuanza kwa mahojiano hayo leo.
 
“Ni kweli mahojiano yanaanza leo, sikumbuki ratiba ya majina ya wale watakaoanza kuhojiwa kwa sababu ratiba iko ofisini, lakini ninavyofahamu wataanza watuhumiwa wa sakata la Escrow,” alisema Barongo.
 
Wakati akina Chenge wakihojiwa, Jaji Mkuu Mohammed Othman Chande, amesema umakini, taratibu na sheria zinahitajika katika uchunguzi dhidi ya majaji wanaodaiwa kupewa mgawo wa fedha za akaunti hiyo.
 
Pia, ameahidi kuweka hadharani kwa umma matokeo ya uchunguzi huo na kwamba mahakama itafanya hivyo kwa kuwa wananchi wanashauku na haki  ya kujua hatma ya uchunguzi dhidi ya majaji hao.
 
Majaji wanaotuhumiwa katika sakata la Escrow ni wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Prof. Eudes Ruhangisa,  anayedaiwa kugaiwa Sh. milioni 404.25 na Jaji Aloysius  Mujulizi anayedaiwa kugaiwa Sh. milioni 40.4.
 
Hata hivyo, Jaji Mkuu Chande, hakuweka wazi uchunguzi huo unaoendelea unatarajiwa kumalizika lini, ingawa alisisitiza kwamba wananchi watapewa taarifa.
 
“Uchunguzi dhidi ya majaji unachukua muda, lazima twende taratibu na siyo haraka ili tusikiuke taratibu na sheria, ni lazima tufuate hivyo, tutawajulisha wananchi kwa kuwa ni haki yao kujua. Tunalishughulikia suala hilo kwa wakati na tunaona umuhimu limalizike,” alisema.
 
Jaji Mkuu Chande, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya uzinduzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ambao pia waliadhimisha miaka 60 ya chama hicho, mjini Arusha mwishoni mwa wiki.
 
Akitolea mfano katika  uchunguzi dhidi ya aliyekuwa Naibu Jaji Mkuu wa Kenya, Nancy Baraza, alisema ulichukua miezi sita kukamilika na kwamba Rais Mwai Kibaki wa nchi hiyo wakati huo 2012 alimteua aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Augustino Ramadhan, kuongoza jopo la majaji waliochunguza kashfa iliyomkabili.
 
Alitoa mfano mwingine wa Tume ya Uchunguzi ya Kikatiba iliyokuwa chini ya Jaji Mark Bomani kuwa, uchunguzi ilioufanya ulichukua mwaka mmoja kukamilika.
 
Akizungumzia hatua za uchunguzi dhidi ya majaji hao wanaotuhumiwa katika sakata la Escrow, alisema umeanza kwa Kamati ya Maadili ya Majaji, halafu utafanywa na Tume ya Utumishi wa Mahakama na kufuatiwa na Tume ya Uchunguzi ya Kikatiba na mwisho atapelekewa Rais ambaye ndiye anayeteua majaji kwa uamuzi.
 
Kashfa ya Escrow imesababisha baadhi ya watuhumiwa kujiuzulu nyadhifa zao na wengine kuvuliwa madaraka, akiwamo Prof. Tibaijuka ambaye pia ni Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), aliyetimuliwa kazi na Rais Jakaya Kikwete, Desemba mwaka jana.
 
Chenge ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, aliachia wadhifa huo wakati Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala) na Mwambalaswa (Lupa-CCM), walilazimishwa kujiuzulu.
 
Mahojiano hayo yatafanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam na yatakuwa ya wazi kutoa fursa mwananchi yeyote kushuhudia.
 
Watuhumiwa wengine wa kashfa ya Escrow watakaohojiwa ni pamoja na majaji na wakurugenzi.
 
 Chenge na Prof. Tibaijuka kila mmoja alipata mgawo wa Sh. bilioni 1.6 kutoka kwa James Rwegamalira wa VIP Engineering and Marketing Limited, zikiwa ni mgawo wa Tegeta Escrow,
Ngeleja alipata mgawo wa Sh. milioni 40.4. 
 
 Mwambalaswa, alilazimishwa kujiuzulu kutokana na kamati yake kushindwa kuisimamia Wizara ya Nishati na Madini.
 
Viongozi wengine waliopata mgawo katika akaunti hiyo ni aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk. 
 
Enos Bukuku (Sh. milioni 161.7)  na Mkurugenzi wa Wakala wa Usajili na Ufilisi (Rita), Philip Saliboko (Sh. milioni 40.4).
 
 Wengine ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Ole Naiko (Sh. milioni 40.4), Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Lucy Appollo (Sh. milioni 80.8). 
 
Ofisa Sheria Mkuu wa tume hiyo, Filotheus Manula, alisema wao wamewafikisha watuhumiwa hao katika baraza hilo kulingana na sheria ya maadili ya viongozi wa umma inavyosema.
 
 “Kama sheria inavyosema, tunapopata malalamiko, tunapeleka mbele ya Baraza la Maadili ambalo huamua ni adhabu gani mtuhumiwa anaweza kuchukuliwa kulingana na sheria inavyosema na kulingana na namna atakavyokutwa na hatia,” alisema na kuongeza:
 
 “Ndivyo itakavyokuwa kwa hawa, kama watakutwa na hatia baraza ndilo litaamua wapewe adhabu gani kulingana na sheria ya maadili ya viongozi wa umma inavyosema.”
 
 Manula alisema Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1993, kifungu cha (8), kinasema kati ya adhabu ambazo viongozi wa umma wanaweza kuchukuliwa pale wanapobainika wamekiuka sheria za utumishi wa umma ni pamoja na kuonywa, kushushwa cheo na kusimamishwa kazi.
 
 Nyingine alisema ni kufukuzwa kazi na kushauriwa kujiuzulu; na kwamba hatua nyinginezo ambayo baraza linaweza kuwachukulia baada ya kuwakuta na hatia ni kuwafikisha mahakamani.
 
Prof. Tibaijuka alifukuzwa kazi na Rais Jakaya Kikwete Desemba mwaka jana wakati Chenge alijiuzulu Uenyekiti wa Kamati yake.
 
 Katika sakata hilo, wengine ambao hawahusiki katika shauri la baraza hilo ambao walipata mgawo huo ni viongozi wa umma wastaafu ambao ni Daniel Yona ambaye alikuwa Waziri wa zamani wa Nishati na Madini (Sh. milioni 40.4) na Mbunge mstaafu wa Sumbawanga, Paul Kimiti (Sh. milioni 40.4).
 
 Kadhalika, wengine ambao siyo watumishi wa umma waliohusika katika mgawo huo ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Katoliki la Dar es Salaam Eusebius Nzigilwa (Sh.milioni 40.4), Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini (Sh. milioni 80.8) pamoja na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh. milioni 40.4).
 
 Aidha, vigogo hao wanahojiwa wakati tayari kuna maofisa kadhaa wa serikali ambao wamepandishwa kizimbani kwa kuhusika kwenye sakata hilo.
 
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa