Home » » SUMATRA WAANZA KUDHIBITI NAULI, AJALI

SUMATRA WAANZA KUDHIBITI NAULI, AJALI

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imeanza mikakati ya kudhibiti kupandishwa kwa nauli wakati wa sikukuu za mwisho wa mwaka nchi nzima pamoja na kudhibiti ajali.
Mkakati huo ni kufanya ukaguzi wa mabasi yote katika vituo vikuu vya mabasi, njiani na katika vituo vikuu mikoani kwa kushirikiana na polisi wa Usalama Barabarani ambapo katika ukaguzi waliofanya jana alfajiri katika Kituo cha Ubungo wamekamata magari matano na kuyatoza faini.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mabasi katika kituo hicho cha Ubungo, Ofisa Mawasiliano Mwandamizi wa Sumatra, Maria Mselemu alisema ukaguzi huo ni endelevu hadi mwezi Januari baada ya wanafunzi kurejea mashuleni.
Alisema katika ukaguzi huo wanatoa namba za simu za Sumatra sanjari na kutoa matangazo katika vyombo vya habari kukata tiketi mapema siku nne kabla ya safari ili kuondoa usumbufu.
Alisema pia katika Ofisi ya Polisi wa Usalama Barabarani Ubungo wameweka bei za nauli stahili ili kuhakikisha abiria hawabugudhiwi.
Ofisa Mfawidhi Kanda ya Mashariki wa Sumatra, Conrad Shiyo alisema katika ukaguzi wa magari waliofanya jana asubuhi , wamekamata magari matano ambayo yameanza kutoza nauli za juu kuelekea msimu wa sikukuu.
Alisema Mamlaka hiyo na Kitengo cha Polisi Barabarani imejiwekea utaratibu wa kukagua kwa kushtukiza ili kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinafuatwa.
Shiyo alisema magari yaliyohusika na hujuma hizo ni yale yanayofanya safari zake Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kaskazini ambako abiria wengi husafiri kwa ajili ya sikukuu za mwisho wa mwaka.
Alisema baada ya kuyakam ta magari hayo waliyatoza faini kuanzia Sh 100, 000 hadi Sh 250,000 na kuwaamuru wahusika kuwarudishia abiria kiasi cha fedha walichozidisha.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa