Home » » MADIWANI ITILIMA WAKATAA MIRADI

MADIWANI ITILIMA WAKATAA MIRADI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
MIRADI 60 ya hifadhi mazingira iliyopo katika vijiji 8  vya Wilaya ya Itilima, mkoani Simiyu yenye thamani ya sh bilioni moja, imekataliwa na madiwani wa wilaya hiyo.
Miradi hiyo mikubwa ya hifadhi mazingira bonde la Ziwa Victoria awamu ya pili (LIVEMP II) imeendelea kukataliwa kwa kile kinachodaiwa wananchi kunyang’anywa maeneo yao.
Hali hiyo ilijitokeza katika semina iliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Livemp, wilayani Itilima ambapo baadhi ya viongozi hao wakiwemo madiwani walisema  mradi huo hauna faida kwa wananchi.
Walieleza wananchi wao mbali na kunyang’anywa maeneo yao, elimu ya umuhimu wa mradi huo haijatolewa kwa kiwango cha kutosha ikiwa pamoja na fidia kwa walionyang’anywa maeneo yao.
“Mradi huu wa hifadhi mazingira upo kisiasa, na kwamba wananchi wa maeneo ambayo miradi hiyo inapita hawajapatiwa msaada wowote, hata kuwapelekea miti ya matunda, ili waache kulima katika kando ya mito na badala yake wamenyang’anywa maeneo hayo bila ya kupewa fidia,” alisema Diwani Nestuta Mlyandengu.
Awali akizungumza katika mradi huo kwa niaba ya mkurugenzi wa shirika hilo, Nesphory Subira, alisema mradi huo utawasaidia wananchi wa maeneo wanayopitiwa na miradi hiyo kwa kuwa watapatiwa miti ya matunda kwa ajili ya kupanda kando kando ya mito pamoja na miti mingine kwa ajili ya kuhifadhi mazingira.
Mkuu wa wilaya hiyo, Geogina Bundala, alishangazwa na hatua ya madiwani hao kuikataa miradi hiyo ambayo ingewasaidia wananchi katika kuwaondolea umasikini.
Chanzo:Tanzania Daima 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa