Home » » Wakulima, wafugaji wampongeza Kamani

Wakulima, wafugaji wampongeza Kamani

WAZIRI wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus KamaniWAZIRI wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani, amepokewa na ujumbe mzito kutoka kwa Chama cha Wavuvi na Wafugaji waliofika mkoani hapa.

Dk. Kamani juzi alifanyiwa sherehe za kupongezwa zilizoandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Busega kwa kushirikiana na Mkoa wa Simiyu baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa waziri wa wizara hiyo.
Akiwa katika Kata ya Mkula, Chama cha Wavuvi Mkoa wa Mwanza walimwelezea waziri changamoto mbalimbali zinazowakabili zikiwemo za rushwa ndani ya wizara hiyo.
Akieleza changamoto hizo kwa niaba ya wavuvi wenzake wa Mwanza, Robert Sijaona, alisema wao wana nia ya dhati na serikali, lakini wapo wanyonyaji wachache wanawaangusha kwa kuwakandamiza.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni uvuvi haramu unaotokana na wavuvi hao kutumia mabomu na nyavu haramu.
Alisema ujambazi unaowaumiza ni ule uliokithiri katika Ziwa Victoria ikiwa ni pamoja na kuporwa nyavu zao pamoja na boti za uvuvi.
“Sisi wavuvi tukiwezeshwa tunaweza tutapambana saa 24, hivyo tunaamini kuwa mkombozi wa wavuvi wetu ni wewe Dk. Kamani na tuna imani utatuinua,” alisema Sijaona.
Alisema changamoto nyingine ni katika rushwa kwa wafanyabiashara wakubwa kutokana na kuwakandamiza wafanyabiashara wadogo.
Pia walimwelezea Dk. Kamani kuwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa soko nje ya nchi huku wakieleza endapo wakipata soko  kiurahisi wao ni matajiri wakubwa.
Naye Brida Mshota kutoka katika Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT)   nao walielezea changamoto yao kuwa ni kukosa elimu na faini kubwa endapo wakifikishwa mahakamani na kwamba hawana watetezi.
Pia alisema maeneo ya wananchi yamechukuliwa na serikali ikiwa ni pamoja na maeneo aliyoyataja kuwa ni pori la Maswa, Bunda, Bariadi na mapori mengine.
Akijibu,  Waziri Kamani alisema kuwa atajitahidi kadiri ya uwezo wake kuhakikisha matatizo yanapungua  au kwisha kabisa.
Dk. Kamani alisema wakati anaingia wizarani hapo amekuta kuna changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na wafugaji na wakulima kufikia wakati hata kuuana.
Alisema ameagiza watendaji wa wizara kuwasiliana na watendaji wa wilaya kufahamu matatizo mbalimbali yanayowapata katika maeneo.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa