WAZIRI wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani, amesema
atapambana na majambazi na wanaodhulumu wavuvi na wafugaji ili
kukomesha tabia hiyo.
Alisema hayo juzi alipokuwa akiwahutubia mamia ya wananchi waliofika
katika viwanja vya Lamadi kwa ajili ya mapokezi baada ya hivi karibuni
kuchaguliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa waziri wa wizara hiyo.
Kamani alisema atahakikisha anazunguka maeneo mbalimbali nchini, ili
kubaini watu wanaowanyonya wafugaji, wavuvi na kushughulika nao huku
akiongeza kuwa hakuna sababu ya watu hao kuwa maskini wakati kuna
rasilimali za kutosha.
“Nashangaa sana kwanini nchi iwe maskini, kwanini wafugaji wawe
maskini au wavuvi wawe maskini wakati tuna maziwa makubwa, kama vile
Natron, Victoria, Eyasi, Nyasa, Tanganyika na mito huku kukiwa na
mifugo mingi, lakini wanaohusika na rasilimali hiyo wakiendelea kuwa
maskini zaidi. Hili jambo haliwezani,” alisema.
Kamani ambaye pia ni mbunge wa Busega, alisema ametokea katika
familia ya wavuvi na wafugaji, na kwamba hiyo kazi ataiweza kwa
kuifanya kwa vitendo, hivyo Watanzania wanatakiwa kumpa moyo na nguvu
ili aweze kufanya kazi inavyotakiwa.
Alieleza kuwa yeye si kiongozi wa maneno, anachohitaji ni vitendo na
utekelezaji, hivyo hatomvumilia kiongozi anayeendekeza malumbano na
wizi wa fedha katika idara yoyote inayomuhusu kuisimamia hata katika
halmashauri anayotoka.
Mbunge wa Kahama, James Lembeli, alisema anamfahamu Dk. Kamani tangu
alivyokuwa naye Tanapa, na kwamba kama rais angemchagua ‘mzigo’
asingetokea kumuunga mkono na kumpokea jimboni kwake
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment