Home » » Wakulima Maswa waiunga mkono TACOGA

Wakulima Maswa waiunga mkono TACOGA

SIKU chache baada ya Chama cha Wakulima wa Pamba (TACOGA) kuanza kukusanya saini za wakulima wa zao hilo wilayani Bariadi, Simiyu kwa lengo la kuwasilisha rasmi madai yao kwa serikali na Bodi ya Pamba ili kulipwa fidia kutokana na kuuziwa mbegu za pamba zilizogoma kuota, kimeungwa mkono na wakulima wa pamba wilayani Maswa.
Wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea baadhi ya vijiji kujionea hali halisi ya mbegu za pamba zisizo na manyoya
zinazozalishwa na Kampuni ya Quton Tanzania Ltd ambazo hazijaota shambani, walisema ni vizuri serikali na Bodi ya Pamba ikawalipa fidia kwa kuwa walikuwa wakiipigia debe kuwa ni nzuri.
“Ni vizuri TACOGA wakafika wilayani Maswa kukusanya na saini zetu ili tulipwe fidia na serikali pamoja na Bodi ya Pamba kwani hawa ndio walikuwa mstari wa mbele kututaka tununue mbegu hiyo,” alisema Mwagisu Mboje, mkazi wa Kijiji cha Zebeya.
Walisema zao la pamba limekuwa halina tija kwa mkulima, kwani hawana maamuzi kila jambo wamekuwa wakipangiwa kuanzia kulima hadi kwenye soko, jambo linalowakatisha tamaa kuendelea kulilima. Pia waliitaka serikali kuivunja Bodi ya Pamba, kwani haina manufaa kwa mkulima.
“Kuna haja gani ya kuwepo kwa Bodi ya Pamba ambayo imekaa kumnyonya mkulima tu na serikali haiivunji, sie tunabaki masikini lakini wao wananeemeka?” alihoji Nyanjige Nkongolo, mkazi wa Kijiji cha Mwabayanda.
Kumekuwepo na malalamiko ya wakulima wengi wa zao la pamba katika mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Geita na baadhi ya wilaya za Mkoa wa Tabora kulalamikia mbegu hizo zilizosambazwa na Kampuni ya Quton kugoma kuota.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa