KATIBU
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willbrod
Slaa, amesema chama chake kikiingia madarakani mwaka 2015 kipaumbele cha
kwanza kitakuwa ni kuuza ndege ya rais ambayo inatumiwa na Rais Jakaya
Kikwete, ili kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Katibu huyo
alisema hayo juzi wakati akihutubia wananchi wa Wilaya ya Bariadi
mkoani Simiyu ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa mikutano ya M4C
Operesheni Pamoja Daima.
"Kipaumbele kingine ambacho kipo katika
ilani ya chama chetu ni kuhakikisha tunauza ndege ya Rais ya sasa
iliyopo na kununua ndege itakayokuwa na uwezo wa kutua kila sehemu,"
alisisitiza Dkt. Slaa.
Alisema hatua hiyo inalenga kutatua changamoto zinazowakabili katika maeneo mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Dkt. Slaa alisema mishahara ya askari wenye vyeo vidogo ni midogo, hivyo haiwezi kukidhi mahitaji yao.
Alisisitiza
kuwa mishahara ya askari hao imekuwa midogo sana kulingana na kazi
wanazozifanya, huku posho zao za kila wiki zikiwa hazikidhi mahitaji yao
kutokana na kuwa ndogo hali inayosababisha askari hao kushiriki vitendo
vya rushwa.
Alisema jeshi la polisi limekuwa likijihusisha na
vitendo vya rushwa kwa kuwakamata wauza gongo, pamoja na watu wenye dawa
za kulevya kutokana na mishahara yao kuwa ya chini.
Alimtaka Mkuu
wa jeshi la polisi nchini IGP, Ernesti Mangu, kuhakikisha askari hao
wanaachana na vitendo vya rushwa kwa kuwaongezea mishahara, pamoja na
kuacha tabia ya kutumia kauli za kijeshi.
Aidha, Dkt. Slaa
alibainisha kuwa Tanzania inakabiliwa na janga la kuwa na vijana wengi
wa mitaani hali inayohatarisha maisha ya wananchi wengine kutokana na
vijana hao kutokuwa na kazi yoyote, huku akilaumu Serikali kwa kushindwa
kutatua kero hiyo
Chanzo;Majina
0 comments:
Post a Comment