WANANCHI WA wa Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu, wamemkataa
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Hilda Lauwo na Mwenyekiti wa
Halmashauri, Stephen Dwese kwa madai ya kukwamisha maendeleo.
Tukio hilo lilitokea juzi katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo
katika kikao cha pamoja cha majumuisho ya ziara ya siku mbili ya Naibu
Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey
Mwanri, aliyoifanya wilayani hapa na kuwashirikisha wadau mbalimbali.
Wananchi walitoa dukuduku hilo baada ya Naibu Waziri huyo kuwapa
nafasi ya kuuuliza maswali na kutoa maoni yao juu ya uendeshaji wa
halmashauri hiyo.
Walilalamikia uongozi mbovu wa mkurugenzi Lauwo, ambao umesababisha
shughuli za maendeleo kutofanyika kwa kiwango kinachotakiwa huku
wakimtupia lawama Mwenyekiti Dwese kuwa ndie chanzo cha mambo yote
kutokana na kumkumbatia mkurugenzi huyo.
Kutokama na hali hiyo, wananchi hao walimtaka Naibu Waziri huyo akiondoka Maswa aondoke nao, kwani hawawafai.
“Naibu Waziri ukimaliza ziara yako hapa Maswa uondoke na mkurugenzi
na mwenyekiti wa halmashauri kwani hawa ndio wanaokwamisha shughuli za
maendeleo wilayani kwetu. Mkurugenzi ana kiburi na jeuri na hii yote
inatokana na kukingiwa kifua na Mwenyekiti Dwese, mie nadai zaidi ya sh
milioni 30, nilijenga vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi
Igongwa sasa ni miaka 11 nazungushwa na viongozi hawa,” alisema Edward
Bunyongoli huku akishangiliwa na wananchi.
Walisema licha ya halmashauri kupata hati safi, lakini kwa hali
halisi Mkurugenzi Lauwo hana mahusiano mazuri na baadhi ya wakuu wa
idara, jambo linalosababisha shughuli za maendeleo kutokusonga mbele.
Hata hivyo, Mwenyekiti Dwese alipotakiwa kutolea ufafanuzi jambo hilo
na Naibu Waziri, alijikuta akijibiwa kwa sauti na kelele za wananchi
waliohudhuria mkutano huo kuwa ni mwongo huku wakisisitiza aondoke nao.
Akijibu hoja hizo, Mwanri alieleza kushangazwa na baadhi ya viongozi
kutojali kero za wananchi hali ambayo inawafanya wanachi waichukie
serikali.
“Nataka niwaeleze bayana kuwa ukiona unasemwa au unalalamikiwa huo
ndio wakati wa kusikiliza na sio kuwachukia wanaokulalamikia…
nawapongeza wananchi wanaoeleza wazi udhaifu wa viongozi, mambo haya
yasiposhughulikiwa ndiyo yanayosababisha wananchi kuichukia serikali,”
alisema.
Hata hivyo, alikanusha madai kuwa na undugu na Mkurugenzi Lauwo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment