na Samwel Mwanga, Simiyu
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Tabora
imemhukumu, Njile Ntemba (37), mkazi wa Kijiji cha Mwagai, Wilaya ya Meatu,
Mkoa wa Simiyu, kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kuua kwa
kukusudia.
Akitoa hukumu hiyo jana katika
Mahakama ya Wilaya ya Maswa, Jaji wa mahakama hiyo, Haruna Songoro, alisema kuwa
upande wa mashitaka umethibitisha bila kuacha shaka kuwa mtuhumiwa alitenda
kosa hilo.
Ntemba alipatikana na hatia hiyo
baada ya kushitakiwa kwa kumuua, Magreth Benjamin (55), mkazi wa kijiji hicho
ambaye alikuwa mkwewe, kwa kumkatakata kwa mapanga, tukio lililotokea majira ya
saa 8:00 usiku, Agosti 18, 2007.
Ilidaiwa mahakamani hapo mbele ya
Jaji Songoro na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Denis Kamara, kuwa mshitakiwa
alimvamia marehemu nyumbani kwake wakati amelala na kumkatakata kwa mapanga,
hatua iliyosababisha kifo.
Wakati huo huo, Mahakama Kuu Kanda
ya Tabora inayoendelea na kikao chake katika mahakama ya wilaya hiyo
imemhukumu, Sami Clement (32) kifungo cha miaka tisa jela baada ya kupatikana
na hatia ya kuua bila kukusudia.
Ilidaiwa kuwa mshitakiwa alimuua
Tiho Shagembe (70) mkazi wa Kijiji hicho kwa kumpiga na jembe kichwani na
kumsababishia kifo baada ya kumtuhumu kuwa ni mshirikina.
Tukio hilo lilitokea Mei 16, 2007
katika Kijiji cha Gambosi, Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu.
Akitoa hukumu hiyo, Jaji Haruna Songoro alisema
kuwa upande wa mashitaka umethibitisha kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo na
adhabu hiyo iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hiyo.
CHANZO TANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment