Home » » Wajasiliamali waliokopa pesa za wamarekani washindwa kurejesha, Sasa kuburuzwa mahakamani

Wajasiliamali waliokopa pesa za wamarekani washindwa kurejesha, Sasa kuburuzwa mahakamani

WAJASILIAMALI 120 walioko katika wilaya za Busega na Magu, waliokopeshwa kiasi cha sh. 72 milioni kwa masharti nafuu na shirika moja lisilokuwa la kiserikali la Rural Initiatives and Relief Agency (RIRA) lililofadhiliwa na serikali ya Marekani, wameshindwa kurejesha fedha hizo na sasa shirika hilo litawafikisha mahakamani.

Mkurugenzi wa shirika hilo lenye makao yake makuu katika katika kijiji cha Kabita wilayani Busega, mkoani Simiyu, Bw. Johnson Rollas, amesema kuwa watu hao walikopeshwa fedha hizo mwaka juzi na walitakiwa kuzirejesha mwezi septemba mwaka jana ili wananchi wengine waweze kukopeshwa.

Bw. Rollas amesema kuwa wananchi hao wakiwemo maafisa watendaji wa vijiji na kata, wenyeviti wa vitongoji na mitaa na wanachama wa vikundi wa wajasiliamali walikopeshwa pesa hizo kwa ajili ya kufanyia biashara ndogondogo, ikiwa ni pamoja na kilimo cha bustani, ufugaji wa kuku pamoja na upandaji miti, baada ya kuweka dhamana ya mali zao zisizohamishika yakiwemo mashamba na nyumba.

Amesema kuwa wananchi hao walikopa mikopo hiyo kati ya shilingi milioni moja hadi milioni tatu na kwamba fedha hizo zilitakiwa zirejeshwe kwa riba ya asilimia tano na kisha kukopeshwa watu wengine na baadaye kurejeshwa kwa wafadhili hao baada ya awamu hiyo ya kwanza kuwa imemalizika.

Aidha, mkurugenzi huo amesema kuwa watanzania hao wameliabisha taifa kwa kukopa fedha za wafadhili na kushindwa kuzirejesha na kwamba sasa shirika lao linaiomba serikali kuingilia kati, ili wakopaji hao waweze kurejesha fedha hizo ndani ya siku 14 kabla ya kufikishwa mahakamani.

Amesema kuwa serikali ya Marekani imeshindwa kutoa fedha nyingine kwa shirika hilo kutokana na wakopaji hao kutokurejesha fedha hizo za kwanza na hivyo kufanya shirika lao kutokuaminiwa na wafadhili hao.

Ameongeza kuwa iwapo wananchi hao wakishindwa kurejesha pesa hizo kwa muda ambao ni wanyongeza wa siku 14, utakapokuwa umeisha watapeleka suala hilo mahakamani na kwamba mali zao walizoweka dhamana zinaweza kuuzwa na hivyo hali hiyo inaweza kuleta mtafaruku mkubwa katika jamii na familia zao kwa ujumla.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa