na Samwel Mwanga, Simiyu
WANANCHI Mkoa wa Simiyu wanaotumia umeme wamelikumbusha Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuanza kuchukua tahadhari za mvua za El-nino zilizotabiriwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu katika maeneo ya Kanda ya Ziwa ukiwemo mkoa wa Simiyu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima jana, wananchi hao walisema ili kuondoa kero ya mara kwa mara ya kukatika umeme, shirika hilo linapaswa kufanya matengenezo na marekebisho katika maeneo korofi ikiwemo kuchimbia nguzo ambazo zina dalili ya kudondoka.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hilo umebaini hali ya njia ya umeme kutokea kituo cha gridi ya umeme cha Ibadakui Manispaa ya Shinyanga kuelekea wilaya za Kishapu mkoani Shinyanga, Lalago wilayani Maswa kuelekea Sanga Mwalugesha hadi mjini Mwanhuzi wilayani Meatu kuwa katika hali ya mashaka ya kudondoka.
Hali hiyo pia iko katika njia inayopeleka umeme kutoka Lalago wilayani Maswa kuelekea mjini Maswa, Luguru hadi mjini Bariadi na maeneo ya viwanda vilivyoko Nyakabindi.
“Umeme unapokatika mara kwa mara huwa tunapata shida katika kufanya shughuli za kujipatia riziki, tunaiomba TANESCO kulishughulikia tatizo hili sasa,” alisema mkazi wa mjini Bariadi, Masanja Matondo.
Kwa upande wake, Jon Sangijo alisema wamekuwa wakifanya jitihada za kujikwamua na umaskini, lakini tatizo kubwa limekuwa ni umeme ambao umekuwa ukikatika mara kwa mara hasa katika kipindi cha masika.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa shirika hilo, Matya Katondo, amekiri kuwepo na kutokea kwa matatizo hayo hata hivyo amedai kuwa shirika linajipanga kukabiliana na hali hiyo na kuahidi hatua za awali zitaanza kuchukuliwa wakati wowote kuanzia sasa.
Katondo alisema katika hatua za awali tayari nguzo za dharula zimeanza kupelekwa katika maeneo korofi ikiwemo wilaya za Kishapu mkoani Shinyanga na Meatu katika mkoa wa Simiyu na kwamba Maswa zimepelekwa nguzo 20 zinazotarajiwa kusimikwa katika njia inayoelekea Lalago, Sayusayu na Malampaka.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment