Home » » WAUAWA KIKATILI KWA IMANI ZA KISHIRIKINA

WAUAWA KIKATILI KWA IMANI ZA KISHIRIKINA

na Samwel Mwanga, Simiyu
WATU wawili wameuawa kikatili kutokana na imani za kishirikina katika wilaya za Bariadi na Maswa mkoani Simiyu akiwamo kijana mmoja kuchinjwa kichwa, kunyofolewa sehemu zake za siri na kuchukuliwa kwa unyao wa mguu wa kushoto.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Salumu Msangi, alisema kuwa mauaji hayo ya kutisha yametokea usiku wa kuamkia juzi majira ya saa 2:00 usiku katika Kijiji cha Ikinabushu Kata ya Gilya, Tarafa ya Dutwa  wilayani Bariadi.
Alisema kuwa kijana huyo anayedhaniwa kuwa na umri wa miaka kati ya 25 hadi 30 aliuawa kikatili na watu wasiojulikana na mwili wake uligunduliwa na wananchi baada ya kutelekezwa.
Alisema kuwa kijana huyo anaonekana kutekwa kutoka kijiji kingine na kufikishwa katika eneo hilo kwa lengo la kupoteza ushahidi.
Kamanda  huyo alisema kuwa amewaomba wananchi kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili kuweza kubaini wauaji hao.
Katika tukio jingine, kikongwe mmoja aliyefahamika kwa jina la Minza Hongo (72) mkazi wa Kijiji cha Mwandu, Kata ya Kulimi, Tarafa ya Sengerema wilayani Maswa ameuawa kikatili kwa kupigwa na rungu kichwani hadi kufa.
Tukio hilo lilitokea Agosti 21, mwaka huu majira ya saa 2:00 usiku katika kijijini hicho wakati ajuza huyo akiwa amelala ndani ya nyumba yake.
”Watu wasiojulikana walivunja mlango wa nyumba yake ka kutumia jiwe kubwa maarufu kwa jina la ‘fatuma’ na kumshambulia kikongwe huyo kwa marungu kichwani na kuvuja damu nyingi na kufariki dunia papo hapo,” alisema.
Alisema jeshi hilo linamshikilia kijana mmoja Kinamaguli Bunzali (22) kwa tuhuma za mauaji ya kikongwe huo.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa