MKOA wa Simiyu umedhamiria mwaka huu kuanza kujenga kiwanda cha aina
yake Afrika Mashariki cha kutengeneza bidhaa za afya zinazotokana na
pamba baada ya hatua za upembuzi yakinifu kuelekea kukamilika na michoro
ya ramani ya kiwanda kuthibitishwa.
Akizungumza jana, siku moja kabla ya Jukwaa la biashara kufanyika
mkoani hapa leo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, alisema hatua
hiyo, siyo tu kwamba inalenga kutekeleza mpango wa kujenga Tanzania ya
viwanda, lakini pia itasaidia katika kuongezea thamani ya zao la pamba.
Mkoa wa Simiyu ndio unaotoa asilimia 60 ya pamba yote inayolimwa Tanzania kwa mujibu wa takwimu za mwaka huu.
“Simiyu tunaongoza kwa kuzalisha pamba nchini, lakini unajiuliza tuna
sababu gani ya hii nchi kuagiza pamba za kusafisha masikio, tuna sababu
gani ya kuagiza bandeji, kuagiza pampasi, kuagiza taulo za usafi wa
akina mama, tuna sababu gani ya kuagiza pamba za kusafishia vidonda?
Hatuna sababu hiyo,” alisema.
Alisema walikaa na kuona ili wazo la kuanzisha kiwanda hicho
kitakachogharimu takribani Sh bilioni 250 lisibaki nadharia wakaamua
kushirikisha wadau na sasa linaelekea kuwa kitu halisi.
Baada ya mkoa kutoa ardhi, Mtaka alitaja wadau wanaoshiriki katika
kiwanda hicho kitakachokuwa pia kinazalisha maji yanayotumika
hospitalini kwa kuwaongeza wagonjwa (dripu) kuwa ni Shirika la Bima ya
Afya (NHIF) litalogharimia ujenzi huku Bohari la Dawa (MSD) likitazamiwa
kuwa mnunuzi mkuu wa bidhaa hizo.
Katika ujenzi huo alisema fedha zinatazamiwa kutolewa na Benki ya TIB
huku Shirika la Viwango (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)
vikihakikisha kiwanda kinatoa bidhaa zenye wezo wa kushindana kimataifa.
Wadau wengine katika mradi huo, Mtaka aliwataja kuwa ni Taasisi ya
Utafiti wa Viwanda na Maendeleo (TIRDO), Shirika la Uhandisi, Usanifu na
Uzalishaji Bidhaa Tanzania (TEMDO), Baraza la Taifa la Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).
“Tunatamani kuona Rais John Magufuli atakapokuwa anasimama mwaka 2020
kuomba tena ridhaa ya Watanzania kuongoza nchi anasema baada ya ujenzi
wa hospitali na zahanati, sasa pia tumeanza kujitosheleza kwenye biadhaa
za hospitali zinazozalishwa kwa pamba,” alisema.
Akiongelea kuhusu jukwaa la uchumi linalofanyika leo mkoani hapa,
Mtaka aliwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje kuja Simiyu kuwekeza na
kutumia vyema sera ya wilaya moja bidhaa moja.
Jukwaa hilo lililoandaliwa na TSN, wachapishaji wa magazeti ya
HabariLeo na Daily News naSpotiLeo, kwa kushirikiana na Mkoa wa Simiyu,
linawakutanisha pia wadau muhimu wa maendeleo kama vile vyombo vya
fedha; Benki za TIB na NMB, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Baraza
la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment