Home » » DKT. SHEIN ASISITIZA WANANCHI KUENDELEA KUPEWA ELIMU YA MPIGA KURA.

DKT. SHEIN ASISITIZA WANANCHI KUENDELEA KUPEWA ELIMU YA MPIGA KURA.

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein akisalimiana na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Simiyu mara baada ya kuwasili uwanja wa sabasaba kutembelea mabanda ya maonesho ya Taasisi na Vikundi mbalimbali vya maendeleo ya vijana wakati wa maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya vijana mkoani humo.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein (katikati) akipata maelezo kuhusu Elimu ya Mpiga Kura  kutoka kwa Afisa Habari Mwandamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bi. Margareth Chambiri mara baada ya kutembelea banda la maonesho la Tume hiyo kwenye viwanja vya sabasaba wilayani Bariadi uemkoani Simiyu.
Baadhi ya Watumishi wa Tume ya Taifa ya Takwimu waliokuwa wakitoa Elimu ya Mpiga Kura wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Mkoani Simiyu. 

Na. Aron Msigwa –NEC, Bariadi-Simiyu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amesema kuwa elimu ya mpiga kura inayoendelea kutolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika maeneo mbalimbali nchini ni vema ikawa endelevu kwa kuwa inaongeza uelewa na kukuza Demokrasia nchini.

Dkt. Shein ameyasema hayo leo mjini Bariadi mkoani Simiyu mara baada ya kutembelea banda la maonesho la Elimu ya Mpiga Kura la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wakati wa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Vijana na kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere mkoani Simiyu.

Amesema hatua ya NEC kuwa na programu endelevu za kuwapatia wananchi elimu ya mpiga katika maeneo yao ni muhimu katika kukuza Demokrasia na kuwafanya waelewe wajibu wao katika kudumisha amani na utulivu nchini kwa kupiga kura kwa uhuru kuwachagua viongozi wanaowataka.

“Hongereni sana, mnapotoa elimu hii mapema mnafanya kazi nzuri, hii inaongeza uelewa miongoni mwa wananchi na kuwafanya  muwafikie wananchi wengi zaidi kabla ya uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020” Amesisitiza Dkt. Shein.

Kwa upande wake Afisa Habari Mwandamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bi. Margareth Chambiri amemweleza Dkt. Shein  kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshiriki maadhimisho ya Wiki ya Vijana mkoani Simiyu ili kutoa Elimu kwa wananchi hususan vijana wa mkoa huo.

“NEC tumeshiriki maadhimisho haya ili kuwaeleza wananchi namna ambavyo chaguzi mbalimbali zinazofanyika nchini zinaendeshwa kwa uhuru na uwazi kabisa, katika kufanikisha jambo hili Idara mbalimbali zimeshiriki ikiwemo Idara ya Elimu ya Mpiga Kura, Idara ya TEHAMA, Idara ya Daftari la Wapiga Kura, Idara ya Uchaguzi na Idara ya Sheria” Ameeleza Bi. Margareth.

Amesema tangu kuanza kwa maonesho hayo Oktoba 8, mwaka huu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imefanikiwa kutoa Elimu ya Mpiga kura kwa wananchi waliokuwa wakilitembelea banda la maonesho la NEC, kutoa elimu hiyo kupitia majukwaa ya wazi ya burudani pamoja na kutoa elimu ya mpiga kura kwa wanafunzi wapatao 2100 wa shule za Sekondari mkoani humo.



0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa