Kareny Masasy, Bariadi MWALIMU Daniel Msalika (42) wa shule ya msingi
Nyasosi, wilayani Bariadi, mkoa wa Simiyu amefariki dunia katika
Hospitali ya Rufaa ya Bugando alikokuwa amelazwa akitibiwa majeraha.
Majeraha hayo yalitokana na kushambuliwa na baadhi ya wananchi kwa
madai ya kujihusisha kimapenzi na wanafunzi wa kike wa shule hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Onesmo Lyanga aliwaeleza waandishi
wa habari jana ofisini kwake kuwa mwalimu huyo alifariki dunia Julai 31
mwaka huu saa nane usiku.
Kamanda Lyanga alisema kuwa siku ya tukio Julai 27 mwaka huu saa 6.30
usiku, wananchi hao ambao idadi yao haijafahamika, walivamia nyumba ya
mwalimu huyo baada ya kupata taarifa kuwa kuna mwanafunzi ambaye amelala
nyumbani kwake, jambo ambalo halikuwa la kweli.
“Wananchi hao walipata taarifa ya kuwa nyumbani kwa mwalimu kuna
mwanafunzi ambaye amelala humo hivyo walimvamia kwa kuvunja mlango na
kuanza kumshambulia kwa kutumia silaha mbalimbali za jadi na
kumsababishia majeraha makubwa sehemu za kichwani na usoni lakini binti
waliyemkuta kwake ni mwenye umri wa miaka 18 na siyo mwanafunzi,”
alisema.
Alisema kuwa baada ya uvamizi huo, mwalimu huyo alikimbizwa katika
Kituo cha Afya cha Isanga kupatiwa matibabu, lakini hali yake iliendelea
kuwa mbaya na kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini
Mwanza, lakini alifariki dunia.
Kamanda alisema kifo chake, kimesababishwa na majeraha ya kushambuliwa huku tuhuma dhidi yake zikiwa si za kweli.
Alitoa mwito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi huku
wakisisitiza kuwa wote watakaobainika kusababisha kifo hicho, sheria
itachukua mkondo wake.
HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment