Home » » KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2015: MAMLAKA YA USAFIRI WA ANGA TANZANIA (TCAA) YAKATAZA KURUSHA CHOPA BILA KIBALI

KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2015: MAMLAKA YA USAFIRI WA ANGA TANZANIA (TCAA) YAKATAZA KURUSHA CHOPA BILA KIBALI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


  1. UTANGULIZI
    1. Tangazo hili linatolewa kwa lengo la kutoa mwongozo kwa watoa huduma za helikopta, marubani wake na umma kwa ujumla kuhusiana na hatua za kiusalama zinazopaswa kuzingatiwa inapolazimika kutoa huduma ya usafiri wa helikopta hapa nchini, hususan, maeneo ya mbali (vijijini) ambapo huduma za uongozaji ndege hazipo au sio maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya helikopta kutua (mahsusi kwa helikopta au viwanja vya ndege kwa ujumla). Tangazo hili limetolewa baada ya Mamlaka kugundua kwamba kumekuwa na matumizi mabaya ya huduma hizi kinyume na kanuni za usafiri wa anga nchini na weledi unaozingatia taratibu za kitaaalamu na miongozo katika usafiri wa anga.
      .
    2. Mamlaka inatambua kwamba matumizi ya helikopta wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 yanatarajiwa kuongezeka na kuna uwezekano wa kuleta athari za kiusalama kwa maisha ya watu na mali pamoja na watumiaji wa vyombo hivi. Pia vitendo vya kuning’iniza vitu kama mabango ya matangazo mbalimbali kwa kutumia ndege (helikopta ikiwemo) yanaweza kuleta hatari endapo sheria na taratibu zinazohusiana na matumizi hayo hazitazingatiwa.
    3. Tangazo hili linatolewa kwa mamlaka aliyopewa Mkurugenzi Mkuu chini ya Sheria Namba 80 ya Usafiri wa Anga na kanuni zake zinazohusiana na masuala ya usafiri wa anga nchini zilizowekwa kwa lengo, hususan, kuhakikisha usalama katika matumizi ya vyombo vya usafiri wa anga sambamba na kulinda usalama wa umma na mali wakati wa matumizi ya vyombo husika.
    4. Watoa huduma za usafiri wa helikopta au ndege na marubani wake wanaokodishwa kutoa huduma wakati wa kampeni, na mtu yeyote anayetarajiwa kutumia huduma hiyo wanakumbushwa kuhakikisha wanazingatia kanuni za usafiri wa anga na ikibidi kuomba kibali kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania. Kanuni zinapatikana kupitia tovuti yetu kwa anuani ya:www.tcaa.go.tz; na endapo utahitaji maelezo ya ziada au miongozo zaidi usisite kuwasiliana na Mamlaka.
  2. CHETI CHA NDEGE KWA USALAMA WA KURUKA – AIRWORTHINESS CERTIFICATE
    1. Helikopta yeyote itakayotoa huduma katika kampeni za kisiasa lazima iwe ina cheti halisi cha usalama wa kuruka kilichotolewa na mamlaka husika ya helikopta ilikosajiliwa. Kwa hapa nchini cheti hicho ni lazima kiwe kimetolewa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga. Na cheti hicho ni lazima kiwe kimetolewa kwa ajili ya helikopta yenye usajili na mahsusi kwa kazi ya kubeba abiria ambayo inaweza kutumika kwa shughuli nyingine zozote. Kwa tangazo hili helikopta nyingine yeyote ile isiyokuwa na sifa hiyo haiwezi kutumika kufanya biashara ya usafiri wa abiria katika kampeni.
    2. Endapo helikopta itakuwa ina usajili wa nje ya Tanzania, mtu anayetarajia kuitumia hapa nchini ni lazima apate kibali cha kuiingiza nchini na kuitumia kwa usajili wa nchi iliyotoka kama ilivyoainishwa katika Waraka wa Mamlaka unaoainisha taarifa za usafiri wa anga – Aeronautical Information Circular (AIC 08/09). Hakikisha unapoomba kibali uwe umekidhi vigezo vya waraka huu ikiwa ni pamoja na kuwasilisha nakala za nyaraka zinazopaswa kuwasilishwa zikiwemo cheti cha usajili wa ndege, cheti cha ndege kwa usalama wa kuruka, cheti cha leseni za radio za ndege, cheti cha bima, makubaliano/mkataba wa kukodisha ndege hiyo, utaratibu wa kufanya matengenezo ya ndege hiyo, leseni za marubani, na ushahidi wa karibuni wa matengenezo ya ndege hiyo.
  3. TARATIBU ZA USALAMA WA UENDESHAJI
    1. Mahitaji ya jumla ya kiuendeshaji

      Matakwa ya marubani na uendeshaji unatakiwa kufuata maelekezo husika yaliyomo kwenye Kanuni inayohusiana na uendeshaji, yaani, The Civil Aviation (Operation of Aircraft) Regulations. Rubani Mkuu anawajibika kuhakikisha kwamba vituo vya Mamlaka vya kuongoza ndege vinavyohusika katika eneo atakalokuwepo au kwa utaratibu wa uongozaji ndege, wanakuwa na taarifa za mpango wake mzima wa safari husika kwa siku au wakati husika.

      Njia itakayotumiwa na rubani izingatie matakwa ya kuepuka kuruka chini ya kiwango cha umbali unaotakiwa hasa katika maeneo yenye watu wengi yakiwemo maeneo yaliyopangwa kufanyika kwa mikutano husika.

      Tahadhari ni lazima zichukuliwe wakati wa kuelekea kutua, kutua kwenyewe na hata wakati wa kuondoka, hasa ikizingatiwa kuwa kuna uwezekano wa wananchi kuikimbilia helikopta au eneo la utuaji. Katika hali yeyote ile rubani hapaswi kutumia chombo chake kukusanya wananchi kwa ajili ya mkutano au kuitumia kwa utaratibu wowote mwingine kinyume na matakwa ya kiurukaji kwa ndege husika.
    2. Usalama wa eneo la kutua na kuruka

      Maeneo yote yatakayotumika kwa ajili ya kutua ama kuruka ni lazima yafahamike mapema. Maeneo ya kuruka ama kutua ni lazima yawe mbali na eneo mkutano utakapofanyika ili kuweza kutoa eneo salama kwa ajili ya kuruka ama kutua kutoka katika mikusanyiko ya watu.

      Maeneo ambayo yatatambuliwa kama ni ya kuruka ama kutua hasa yale ambayo hayajatambulika kisheria kwa kufanyia shughuli hiyo ni lazima yawekewe alama maalum na uzio ili kuzuia watu wasiohusika kusogelea eneo hilo.

      Eneo husika ni lazima lilindwe; rubani mkuu ahakikishe helikopta itakayokuwa imetua eneo hilo inalindwa dhidi ya uvamizi kutoka kwa watu wasiohusika. Hatua maalum za kiulinzi ni vyema kuchukuliwa endapo kutakuwa na ulazima wa chombo hicho kulala katika eneo husika usiku mzima. Kila wakati rubani anapotaka kuruka ni vyema ahakikishe amekagua chombo chake kwa mujibu wa taratibu zinazohusika kwa umakini kabla ya kuanza safari.
    3. Usiamizi wa Chombo kikiwa ardhini na usalama kwa umma

      Mtu mwenye wajibu wa usimamizi wa chombo kikiwa ardhini lazima awe ni mwenye mafunzo ya kutosha na awe anajua madhara yanayoweza kusababishwa na mapanga ya helikopta yanapozunguka. Kwa marejeo zaidi kuhusiaha na hilo tafadhali zingatia yaliyomo kwenye Waraka wa Mamlaka AIC33/2000 unaoelezea masuala ya madhara yanayoweza kusababishwa na mapanga ya helikopta yanayozunguka.

      Ni wajibu wa Rubani mkuu na mhusika aliyekodisha helikopta kuhakikisha wananchi wanakuwa salama na mbali na helikopta. Matumizi ya kizembe na yasiyo ya kiweledi ya helikopta yatakayohatarisha usalama wa wananchi yatachukuliwa kama ukiukwaji wa kanuni za usafiri wa anga na Mamlaka itawachukulia hatua kama ilivyoanishwa kwenye kanuni hizo.
    4. Kuchukua na kuangusha vitu ardhini na kupeperusha mabango angani

      Huduma hizi zinaweza kufanywa na helikopta na hata ndege zingine za kawaida. Kabla ya kufanya shughuli za namna hiyo, mmiliki wa chombo ni lazima ahakikishe anakidhi vigezo vya Kanuni za Usafiri wa Anga kwa huduma hizi, yaani, The Civil Aviation (Aerial Work) Regulations na pia awe amepatiwa kibali kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga kwa kazi hiyo. Mmiliki wa ndege yeyote anayefanya shughuli za namna hii bila ya kuzingatia vigezo vya Kanuni hizi atachukuliwa hatua.
    5. Kutoa taarifa za matukio

      Rubani Mkuu ni lazima aandike taarifa ya matukio na kuiwasilisha Mamlaka ya Usafiri wa Anga kama ilivyoanishwa kwa mujibu wa kanuni za usafiri wa anga hususan, kanuni za 52, 74,75 na 76 zilizomo kwenye Kanuni ya The Civil Aviation (Operation of Aircraft) Regulations. Wananchi nao wanatakiwa kutoa taarifa ya tukio lolote waliloliona hatarishi kwa mujibu wa kanuni namba 262 ya Kanuni iliyotajwa.

      Mamlaka itafuatilia na kuchunguza taarifa inazozipokea na kuchukuwa hatua stahiki ili kuhakikisha kuwepo kwa usalama wa kiuendeshaji, watu na mali.
  4. HITIMISHO
    Ili kulinda usalama wa wananchi, wamiliki na marubani wote wanapaswa kuhakikisha wanazingatia Sheria ya Usafiri wa Anga pamoja na Kanuni zake. Rubani anayeendesha chombo ni lazima ahakikishe anatumia weledi wa hali ya juu katika matendo yake.

    Mamlaka inawahakikishia wananchi/umma kwa ujumla kwamba haitosita kuchukuwa hatua stahiki kama zilivyoanishwa kisheria na kanuni za usafiri wa anga iwapo mapungufu ya usalama yatajitokeza.
Imetolewa na
Charles M. Chacha
Kaimu MKURUGENZI MKUU
MAMLAKA YA USAFIRI WA ANGA TANZANIA

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa