Home » » SOMA HAPA-NANI ANACHEZESHA NGOMA YA ESCROW NA IPTL?

SOMA HAPA-NANI ANACHEZESHA NGOMA YA ESCROW NA IPTL?




Kwa muda sasa kumekuwapo na tuhuma zinazohusu "wizi" wa fedha za akaunti ya escrow iliyofunguliwa katika Benki Kuu ya Tanzania mwaka 2006. Akaunti hiyo ilifunguliwa kwa ajili ya kuhifadhi fedha zilizokuwa zikilipwa na Shirika la Umeme Tanzania {TANESCO} kwa kampuni ya kufua umeme ya IPTL. Chimbuko la akaunti hiyo ni mgogoro wa tozo hiyo kwamba iligubikwa na utata baada ya kudaiwa kwamba Tanesco ilikuwa ikitozwa fedha nyingi kuliko inavyostahili.
           
Tuhuma za huo "wizi" hata hivyo hazikuishia tu kwa wahusika wakuu yaani makampuni ya umeme, bali zimetiririshwa hadi kwa watu binafsi ambao kimsingi hawana uhusiano wowote na mgogoro huo wa malipo na wala kuhusika kwa njia yoyote na hicho kinachodaiwa kwamba ni uporaji wa fedha za akaunti hiyo ya Escrow. 

Akaunti Escrow ni akaunti ya amana ambayo inawekwa chini ya uangalizi wa mtu wa tatu ili huyo mwangalizi aikabidhi kwa mlengwa pale tu masharti kadhaa yatakapokuwa yamekamilishwa. Hivyo basi akaunti hiyo maalum ya amana ilifunguliwa na kuwekwa chini ya Benki Kuu kama wakala anayesubiria kutekelezwa kwa masharti maalumu ili aikabidhi kwa wenye kumiliki fedha hizo watakapomaliza tofauti zao.
          
Ni vizuri kuliangalia suala hili la akaunti maalum ya amana kwa namna ambayo itawafanya wale wenye kiu ya kutaka kujua ukweli kukidhi hamu yao. 

Fedha iliyokuwa ikiwekwa katika akaunti hiyo ni tozo ya uwezo wa mitambo ya kufua umeme ambayo kampuni ya IPTL ilikuwa ikiitoza Tanesco. Baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) kupunguza tozo ya IPTL kutoka USD 3.6million kila mwezi mpaka USD 2.6million kila mwezi baadaye TANESCO ilishauriwa vibaya na wanasheria kwamba tozo hiyo bado ni kubwa kuliko mkataba baina ya IPTL na TANESCO Mei 26, 1995 unavyo eleza.
          
Ubishani uliozuka kati ya mtoa huduma ya umeme yaani IPTL na mtumia huduma ya umeme yaani Tanesco ndio uliosababisha kufunguliwa kwa akaunti hiyo maalum ya amana yaani escrow account katika Benki Kuu ya Tanzania {BoT} kama njia salama ya kutunza fedha hizo hadi mgogoro utakapokuwa umetatuliwa. 

Ni muhimu kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba mtoa huduma yaani IPTL hasitishi kufua umeme na mtumiaji wa umeme yaani Tanesco naye hakosi umeme wa kuuza kwa walaji wake. Hiyo ni busara ya kibiashara. Fedha hizo zililipwa katika akaunti hiyo maalum kutokana na hati za madai au ankara kutoka kwa mtoa huduma na si vinginevyo.
          
Kitu kimoja kilichojitokeza wazi ni kwamba suala la akaunti hiyo maalum limekuwa likibeba sura mpya kila kukicha na la kusikitisha zaidi ni kwamba vyombo vya habari vilivyo vingi ama vimekuwa vikipotosha kwa makusudi au kwa kutokuelewa mada yenyewe ipasavyo. Vipo vyombo vya habari kwa mfano ambavyo vimedai kwamba "Benki ya Standard Chartered ndiyo mmiliki wa mitambo ya IPTL baada ya kupewa mamlaka hayo na mahakama - Deed of Assignment- inayoiruhusu kuchukua na kumiliki mali za IPTL kutokana na kushindwa kulipa mkopo.

Aidha kwa mujibu wa gazeti la Mawio la Alhamisi Novemba 20-26, 2014 mkataba huo uliipatia benki ya SCB haki za IPTL ndani ya mkataba wa kuuziana umeme (PPA) na kumiliki mtambo wa kuzalisha umeme wa IPTL.
          
Kwa mujibu wa gazeti hilo la Mawio Benki ya Standard Chartered inaidai Tanesco dola za Marekani 258.7 milioni kama deni linalotokana na gharama za umeme uliozalishwa na IPTL na dola za Marekani 138 milioni zinazotokana na mkopo pamoja na riba. Kwa mujibu wa uchambuzi wa Mawio madai hayo ni halali kwa mujibu wa sheria.
          
 Kwa mujibu wa gazeti hilo "nyaraka za serikali zinaonesha kuwa PAP iliamuriwa kulipa wadai wote wa IPTL lakini haikuilipa Benki ya Standard Charted ambayo inajitangaza kuwa ni moja ya wadai.
         
Ni vyema na busara kuanza uchambuzi huu kwa kufanya nukuu hiyo muhimu sana kutoka katika gazeti la kila wiki la Mawio kwa sababu inatusaidia kuonyesha waziwazi kwamba hiki kinachodaiwa kwamba ni kashfa ya fedha za Escrow kina sura nyingi sana kulingana na maslahi yanayolengwa kutetewa. 

Katika muktadha huu ni wazi kwamba anayetetewa hapa ni Benki ya Standard Chartered ambayo inadaiwa kwamba ndiyo yenye haki ya kulipwa fedha kutoka katika akaunti ya Escrow na kwa mantiki hiyo imeishitaki Serikali ya Tanzania katika Mahakama ya Uingereza.
          
Deni linalodaiwa kwamba Tanesco inadaiwa na Standard Chartered la dola za Marekani linatokana na gharama za umeme uliozalishwa na IPTL na nyingine ni mkopo na riba. Inashangaza kwamba Tanesco inawezaje kudaiwa na Benki ya Standard Chartered wakati aliyezalisha umeme ni IPTL? Abrakadabra hiyo ndiyo inayomfanya ye yote yule mwenye akili timamu kutambua kwamba kuna mchezo wa kiini macho unaochezwa na benki hiyo dhidi ya Tanzania.
         
Ni wazi kabisa kwamba benki hiyo inalazimisha kuwapo na mgogoro wa kuhusu akaunti ya Escrow kwa lengo moja tu nalo ni kuhakikisha kwamba wanapata nafasi ya kukwapua hizo fedha wanazodai kwamba sio halali kuchukuliwa na IPTL. Kwamba zikichukuliwa na Benki ya Standard Chartered ambayo haijazalisha umeme wala kuwa na ushahidi wowote wa kushiriki katika kuzalisha umeme ni halali kabisa na zikichukuliwa na IPTL ambayo imezalisha umeme na inayo mikataba ya kuuziana umeme na Tanesco si sahihi, ni wizi, ni ujambazi ni hila na kashfa. Hii inahitaji maelezo zaidi kushinda haya yanayotolewa hivi sasa.
          
Ukweli wa mambo ni kwamba mazungumzo kuhusu fedha za Escrow na hususan habari za kujaribu kuonyesha kwamba umiliki wake ni batili una lengo moja tu nalo ni kuandaa mazingira kwa ajili ya Benki ya Standard Chartered hatimaye kuzichukua fedha hizo kwa kutumia kigezo cha kwamba imemilikishwa mitambo ya IPTL na kwamba ndiyo iliyokuwa na haki ya kulipwa tozo ya uzalishaji umeme na si kampuni nyingine yoyote. Hivyo ndivyo kampuni hiyo inavyodai katika kesi iliyofungua dhidi ya Serikali ya Tanzania huko Uingereza.
          
Benki ya Standard Chartered inatumia mbinu mbalimbali ili kuhakikisha inafikia lengo lake la kukwapua fedha za kigeni si chini ya dola milioni 200 kutoka kwa serikali ya Tanzania. Moja ya njia inayotumia ni propaganda ambayo hupenyezwa katika vyombo vya habari kwa kutumia majukwaa mbalimbali. 

Moja ya njia zinazotumika ni kujaribu kuufanya umma uamini kwamba fedha zilizotoka katika ufungaji wa akaunti hiyo ya Escrow zimeibwa na kwamba wahusika katika huo wizi ni pamoja na viongozi kadhaa wa Serikali.
          
Kinachosikitisha zaidi ni kwamba kuhusishwa kwa watu hao kunafanyika bila hata ya kuwataka wajieleze kama wanaelewa kile wanachotuhumiwa nacho. Wafadhili wa propaganda hizo hawakubali kujitokeza hadharani moja kwa moja kwa kuhofia kuumbuliwa. Matukio huchukuliwa si kwa ujumla wake bali upande mmoja na kuyatangaza kwa namna ya kukidhi matakwa na matarajio yao tu.
          
Tumezoea kuambiwa kwamba wakati suala linapokuwa mahakamani kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi basi si sahihi kuendelea kulijadili kwenye vyombo vya habari kwani kwa kufanya hivyo ni sawa kabisa na kuingilia uhuru wa mahakama. Ni wazi kwamba hata suala linapokuwa katika uchunguzi au upelelezi uwe kwa kutumia tume maalum au makachero basi ni muhali kulizungumzia hadharani na kuwatuhumu na hata kuwahukumu watu kwa ujasiri usio na kikomo kwamba ni wezi au mafisadi au wakumbatiaji wa madhila hayo yote. Hili linafanyika kila siku kupitia vyombo vya habari na chimbuko lake ni baadhi ya wabunge na wanasiasa ambao hufanya hivyo huku wakitumia kila aina ya takwimu za kweli na za kughushi au kubuni tu kichwani.
         
Nini kinachowafanya au kuwapa jeuri hawa watu wanaowatuhumu na kuwahukumu wengine bila ya kujali kwamba hilo halitakiwi wala kupaswa kufanyika bila ya kupitia katika vyombo vya sheria ili kutoka fursa kwa wengine kujitetea? Swali hilo linastahili kujibiwa kwa umakini mkubwa ili kubaini kama kweli hao wanaodai kwamba wanapigania haki ya kiuchumi ya Watanzania ni kweli wanafanya hivyo kwa dhati ya moyo wao kabisa bila ya kuwa na nia nyingine iliyojificha ambayo hawathubutu kuiweka hadharani kwani kwa kufanya hivyo watageuka viroja. 

Pamoja na kwamba kuna kesi mahakamani dhidi ya Serikali ya Tanzania ni wazi kwamba ukiwauliza Standard Chartered kilichowapeleka mahakamani wanasema kwamba wanaionea nchi yetu huruma, Hata hivyo, kamwe hakuna atayekuambia kwamba amekuja hapa kwa ajili ya kujaribu bahati yake kama wanaweza kufanya mbinu wakatengeneza fedha ya bure. Ili kufanikisha malengo yao tuhuma hurushwa kwa yeyote na popote. Ili kufanikisha malengo hayo mtu yeyote yule aweza kuunganishwa katika lolote lile ili kufikia lengo.
          
Ni kwa utaratibu huo huo ndio tunashuhudia jinsi jitihada za Profesa Anna Tibaijuka za kuendeleza mtoto wa kike kielimu zinavyopakwa matope na kukejeliwa mno kwa sababu tu ameomba msaada mahali na akaupata. 

Tujiulize inakuwaje wanasiasa wetu wanathubutu kumhukumu Profesa Tibaijuka na kumuita kila aina ya majina machafu. Ametuhumiwa kwamba ni mwizi eti kwa sababu aliomba msaada kwa ajili ya shule ya Babro Johansson ambayo ni kwa madhumuni ya kuwasaidia watoto wa kike kupata elimu. 

Profesa Tibaijuka aliomba msaada kwa barua rasmi miaka kadhaa iliyopita na kampuni hiyo haikuweza kumsaidia mapema kutokana na ukata na ni hivi majuzi hali ilipokuwa njema ndipo ikatoa msaada huo.
         
La kustaajabisha ni kwamba msaada huo haukuwa ni siri na ulitolewa kwa uwazi mkubwa bila ya kificho. Sasa huo ujambazi wa Profesa Tibaijuka umetokea wapi? Kosa lake ni kupatiwa fedha alizoomba kwa ajili ya kuisaidia shule ambayo aliianzisha?
          
Tunajiuliza hapa, baada ya VIP kuuza hisa zake kwa PAP na kulipwa na PAP stahili yake, ilifanya kosa gani kutoa msaada kwa shule ya Babro Johansson?
          
Mahitaji na umuhimu wa elimu yanajulikana. Viongozi wanahimiza kila leo umuhimu wa Watanzania kubadilika kuchangia Maendeleo ya Elimu badala ya harusi na sherehe nyinginezo. Leo hii anatokea Mtanzania anaomba msaada wa kuendeleza elimu na anapatikana Mtanzania anakubali kuchangia vizuri maendeleo ya elimu, wawili hawa baadhi ya wanaojiita viongozi wa siasa tena wenye kutaka kuchukua madaraka ya juu kuiongoza nchi, wanalalamika na hata kutamani kutoa roho ya mtu! Watanzania tuzipime dhamira zao. Ni wadanganyifu wasio na uelewa halisi wa matatizo na vipaumbele vya taifa na hivyo kukosa dhamira thabiti ya kuyashughulikia. Wanasukumwa zaidi na tamaa zao binafsi. 
          
Kwa wanaong'ang'ania kudai damu za baadhi ya watu kutokana na hukumu ambayo wao wameipitisha baada ya kufanya kila kitu wao ikiwa ni pamoja na kutuhumu, kupeleleza, kufungua mashitaka, kusikiliza kesi na hatimaye kuhukumu na sasa kutaka kukaza hukumu kwa njia yoyote ile hakuna jambo zuri na jema kama kufanya kile wanachotaka wao yaani kukubali kwamba fedha zote katika akaunti maalum ya escrow ni za serikali na kwamba lazima zirudi serikalini. 

Hata hivyo, wakubwa hao hawataki kurudi nyuma na kujiuliza ni kwa njia gani fedha hizo zimeingia katika akaunti hiyo. Aidha, hawataki kujiuliza kwamba kama Tanesco ndio ilikuwa ikitumbukiza fedha katika akaunti hiyo, ilikuwa ikifanya hivyo kwa kutumia vigezo gani. Swali linguine la kujiuliza, je Serikali hutunza pesa zake kwenye Account zake Benki Kuu au kwenye Escrow Account?
         
Hawaoni mantiki ya kutulia na kujibu swali la msingi kwamba kama Tanesco ingelikuwa inatumbukiza fedha katika akaunti hiyo kwa ajili ya kugharamia tozo la uwezo wa mitambo kuzalisha umeme sasa inakuwaje fedha hizo zirudi tena Tanesco? Ni maswali ambayo wanaojiamini kwamba ukweli wanao wao tu hawataki kuyajibu hata kidogo kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanaumaliza utamu wa mchezo wao wa kuigiza. 

Fedha hizo zinatakiwa zirudi Tanesco ili Benki ya Standard Chartered izichukue kwa madai kwamba ndiye mmiliki halali wa IPTL na kwamba kuna deni kama ilivyoainishwa awali katika makala haya.
          
Kutokana na ufafanuzi huo hapo juu ni wazi basi kwamba Tanesco ilikuwa ikilipia gharama za huduma ambayo ilikuwa inaipata kutoka kwa IPTL. Hilo halina ubishi.
          
Lakini pia suala lingine ambalo sasa halina ubishi japo halisemwi makusudi kwa sababu za upotoshaji ni kwamba katika makampuni yote ambayo yanauzia umeme TANESCO, IPTL ndiyo kampuni pekee inayotoza kiwango kidogo cha malipo ya uwekezaji (capacity charges). Suala la kujiuliza hapa ni inawezekanaje IPTL ambayo inatoza kiwango kidogo cha capacity charges ionekane “kuiibia” Serikali kwa kulipwa halali yake wakati makampuni mengine yanatoza capacity charges kwa kiwango cha juu zaidi ya IPTL na hakuna malalamiko.
       Swali la kujiuliza ni kwamba ni kitu gani kinachowasukuma watuhumu kutafuta kila njia ya kuonyesha kwamba kuna hitilafu kubwa sana kwa namna ambavyo suala la akaunti hiyo lilivyohitimishwa?
         
Ukifuatilia kwa karibu na umakini jinsi ambavyo tuhuma zimekuwa zikitolewa ni kwamba kinacholengwa ni fedha zilizokuwa katika akaunti maalumu ambazo ni tozo ya uwezo wa ufuaji wa umeme. Fedha hizo zinagombewa na Benki ya Standard Chartered ambayo ina matawi yake hapa nchini. 

Benki hiyo inatumia kila njia kujaribu kuonesha kwamba fedha zilizokuwapo katika akaunti ya Escrow ni fedha ya Serikali. Kwa mantiki hiyo inachojaribu kufanya Benki hiyo ni kuonyesha kwamba fedha akaunti ya escrow si kwa ajili ya kulipia gharama za uwezo wa mitambo kufua umeme la hasha. Bali ni fedha za Tanesco na kamwe hakuna anayestahili kuzipunguza kwa njia yoyote ile.
          
Cha kushangaza, hata hivyo, ni kwamba benki hiyo, inayodai kuwa iliikopesha fedha IPTL, katika madai yake yaliyopo mahakamani, inadai kuwa yenyewe ndiyo ilistahili kupata fedha zilizokuwa kwenye escrow account! Swali hapa ni je, hiyo asasi ndiyo Serikali? Je, fedha zilizokuwa kwenye escrow account zinakuwa za Serikali na siyo IPTL kwa sababu benki hiyo  haijalipwa?
       
Jitihada za kutaka kuhalalisha kwamba fedha hizo ni mali ya Tanesco na kwamba haziwezi kumegwa hata kidogo zinafanywa na Benki ya Standard Chartered ambayo inataka kutengeneza mazingira ya kuchota fedha kutoka Tanesco kwa madai kwamba ndiyo inayostahili kuwa mlipwaji wa fedha hizo kutokana na deni ambalo kwa mujibu wa madai yao ndio walioikopesha IPTL fedha kwa ajili ya mradi huo wa umeme.
          
Mchezo ambao benki hiyo inafanya hapa nchini ni kuhakikisha kwamba vyombo vya habari vinaandika habari za kuigonganisha serikali na wananchi kwamba Serikali ni ya mafisadi na inayokumbatia ufisadi, na haina ubavu wowote wa kupambana na rushwa. Aidha, asasi hiyo imevirubuni baadhi ya vyombo vya habari kuandika habari kwamba Mahakama za Tanzania haziaminiki na zinakumbatia ufisadi na kwamba zimekubuhu kwa rushwa.
          
Cha kushangaza, tuhuma hizi za rushwa kwa Mahakama za Tanzania zinakuja muda mfupi tu baada ya benki ya Standard Chartered kuiambia mahakama New York, nchini Marekani iliposhitakiwa na VIP kuwa Mahakama za Tanzania ndizo zenye uwezo wa kusikiliza na kutatua migogoro ya IPTL.
          
Mchezo ambao Standard Chartered Bank inaufanya ni kutumia vyombo vya habari kutoa habari zisizo za kweli na za upotoshi ili kuwachochea watu dhidi ya Serikali yao kutokana na nini kinaendelea ndani ya IPTL.  Mambo mengi yamesemwa na kuandikwa kuhusiana na Mahakama na watendaji wa Serikali kula rushwa.  Madhumuni ya kufanya hivyo ni kutaka kuonyesha kwamba nchini Tanzania haki haiwezi kutendeka.
         
Madai hayo yote, yanatokea wakati Standard Chartered Bank imefungua kesi London, kwa kisingizio kwamba Mahakama za Tanzania haziwezi kutenda haki  
          
Kwa vipi Standard Chartered Bank inatoa madai kulipwa dola za kimarekani 208 milioni kutoka TANESCO (katika kesi ilivyofunguliwa Mahakama ya usuluhishi (ICSID)) kwa mkopo wa dola milioni 84 kwa IPTL, wakati Serikali ya Tanzania na TANESCO tayari walikwishalipa takribani dola 200 milioni kwa IPTL kufikia mwaka 2006.  Kiasi hicho kingelitosha kulipia mkopo uliokuwa umechukuliwa na kulipa gawiwo kwa VIP na MECHMAR.  Mpaka mwaka 2013 VIP ilikuwa haijalipwa hata senti moja kwa jina lolote.
         
Kampuni ya Mechmar ilitumia fedha zilizodaiwa na IPTL kutoka Serikali ya Tanzania na TANESCO kwa kujilipa yenyewe na Kampuni ya Wartsila madeni hewa (kwa makubaliano na benki ya Danaharta na baadaye Standard Chartered Bank (Hong Kong) Ltd.
         

Standard Chartered Bank (Hong Kong) Ltd inajaribu kutekeleza mpango haramu dhidi ya IPTL kwa kutumia dhamana ya Serikali ya Tanzania na hivyo Serikali ina sababu za kutaka Standard Chartered Bank ithibitishe kama inaidai IPTL.

          Mpaka sasa ukweli ni kwamba Standard Chartered Bank imekwepa kutoa ushahidi kuwa ina madai yoyote dhidi ya IPTL na kwa sababu hiyo na zingine VIP na IPTL/PAP wameifungulia kesi za madai ya fidia na hasara ya TZS 787bilioni na USD 3bilioni katika Mahakama Kuu ya Tanzania. (Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com)

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa