Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mheshimiwa
Paschal Mabiti,kuomboleza vifo vya watu 11 ambao wamepoteza maisha yao
katika ajali ya basi iliyotokea mkoani humo Jumatatu, Aprili 21, 2014.
Katika
salamu hizo, Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuwa
ajali zabarabarani zinaendelea kuchukua maisha ya watu wasiokuwa na
hatia.
“Nimepokea
kwa huzuni nyingi taarifa ya ajali hiyo ambayo nimejulishwa kuwa
imetokea katika Kijiji cha Itwimila katika Wilaya ya Busega katika Mkoa
wako wa Simiyu wakati basi lililokuwa linasafiri kutoka Tarime, Mkoa wa
Mara kwenda Mwanza kupitia Simiyu lilipoacha njia na kugonga nyumba
kabla ya kupinduka.”
Amesema
Rais Kikwete: “Nakutumia salamu zangu za rambirambi na najiunga nanyi
katika kuomboleza msiba huu mkubwa katika nchi yetu. Aidha, kupitia
kwako, natuma salamu za dhati ya moyo wangu kwa familia zote ambazo
zimepoteza wapendwa wao katika ajali hiyo. Naungana nao katika
kuomboleza wapendwa wao. Napenda wajue kuwa msiba wao ni msiba wangu.
Pia, naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema
aziweke peponi roho za marehemu.”
Rais
Kikwete vile vile ametoa pole kwa wote ambao wameumia katika ajali
hiyo, akiwaombea wapone haraka na kurejea kwenye shughuli zao za
kujiletea maendeleo.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
21 Aprili,2014
0 comments:
Post a Comment