na Sitta Tumma, Bariadi
WILAYA
ya Bariadi mkoani Simiyu, imetajwa kuwa ni miongoni mwa wilaya zinazoongoza kwa
wanafunzi wake kuacha masomo na kwenda kuuza pombe za kienyeji na hivyo
kuporomoka kwa elimu wilayani humo.
Mbali
na hayo, imeelezwa kwamba ajira za utotoni, baadhi ya viongozi wa vijiji
kutosimamia vema shughuli za kimaendeleo katika maeneo yao, ushirikiano mbovu
baina ya watendaji na wananchi na makato makubwa ya mishahara ya walimu, ni
chanzo kikuu cha kukwamisha maendeleo.
Kauli
hiyo ilitolewa juzi mjini Bariadi na walimu kutoka sehemu mbalimbali
wanaoshiriki warsha ya siku tatu ya 'Chukua Hatua', iliyoandaliwa na Taasisi ya
Kutetea na Kujenga Demokrasia na Utawala Bora (ADLG).
Wakichangia
mada ya kero katika sekta ya elimu, walimu hao walisema wanafunzi wengi
wamekuwa wakiacha masomo kisha kujihusisha na biashara ya uuzaji wa pombe,
jambo linalodidimiza ukuaji wa maendeleo ya sekta hiyo.
Kwamba
hata baadhi ya viongozi wa ngazi za vijiji na wizara husika wameonekana
kushindwa kuwachukulia hatua za kisheria wazazi wa wanafunzi hao.
Walisema
kuwa ili kuondoa tatizo hilo na hatimaye wilaya hiyo kupiga hatua kubwa za
kimaendeleo, ni vema viongozi wa ngazi zote wakashirikiana pamoja kupambana na
hali hiyo mbaya, ikiwa ni sambamba na kuwachukulia hatua kali za kisheria
wazazi ama walezi wanaoshindwa kusimamia maendeleo ya elimu kwa watoto wao.
“Wanafunzi
wengi wanaingia darasani wakiwa na njaa. Kwa maana hiyo uelewa unakuwa mdogo
sana, maana wengi wanasinzia na kushindwa kusoma vizuri,” alisema mmoja wa
walimu hao.
Aidha
walimu hao walikwenda mbali zaidi na kusema kwamba hulka ya baadhi ya wazazi na
walezi kuwaoza watoto wao wa kike, unywaji wa pombe baina ya walimu wakati wa
kazi ni kikwazo pia cha upatikanaji wa maendeleo, na kwamba baadhi ya wananchi
wa vijiji husika wamekuwa wakiendekeza ubaguzi wa kabila kwa walimu.
Awali,
Mkurugenzi wa ADLG, Jimmy Luhende, alisema lengo la warsha hiyo ni kuwapatia
elimu ya uwajibikaji walimu wa shule mbalimbali katika wilaya sita za mikoa ya
Simiyu, Shinyanga na Geita.
CHANZO MTANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment