na Mwandishi wetu, Simiyu
MKUU wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP-OCS) Joseph Ngeve anadaiwa kumtishia kwa risasi mwendesha pikipiki za abiria kwa tuhuma za kumdharau.
Tishio la mkuu huyo wa polisi limekuja wakati Watanzania wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kifo cha mwandishi wa habari wa kituo cha Chennel 10 kilichosababishwa na kitu kinachoaminika kuwa ni bomu alilopigwa na askari polisi kwenye kijiji cha Nyololo, mkoani Iringa.
Habari za kuaminika kutoka mjini Maswa zinaeleza kuwa tishio hilo lilifanyika hivi karibuni mara baada ya kumalizika kwa kikao kati ya waendesha pikipiki maarufu kwa jina la “bodaboda” na jeshi la polisi kilichoitishwa na halmashauri ya wilaya hiyo chini ya kitengo cha biashara.
Inaelezwa kwamba wakati kikao kikiendelea mwendesha bodaboda huyo (jina limehifadhiwa) alitoka nje baada ya kupata ujumbe mfupi wa maandishi katika simu yake ya kiganjani wa kwenda kumchukua mgonjwa eneo la Njiapanda ili ampeleke hospitali.
Kwa mujibu wa mashuhuda, kitendo hicho hakikumfurahisha ASP huyo aliyedaiwa kukitafsiri kwamba ni dharau aliyoonyeshwa hivyo aliahidi mbele ya kikao kumshughulikia.
“Baada ya mwenzetu kupata ujumbe kwenye simu aliondoka sisi tukiwa ndani ya ukumbi tukiendelea na kikao lakini kitendo hicho kilimuudhi OCS huyo na kuahidi kumshughulikia,” alisema Juma Haji aliyekuwepo kwenye kikao hicho.
Shuhuda mwingine alisema baada ya kikao mwendesha bodaboda huyo alipita na pikipiki yake akiwa na abiria ambaye hana kofia ngumu hivyo kusimamishwa na askari wa usalama barabarani (jina tunalo) na kutakiwa kulipa faini ya sh 30,000 jambo alilotimiza.
Wakati akitaka kulipa faini hiyo ghafla alitokea OCS na kuamuru awekwe mahabusu kwa kilichoelezwa kuwa ni dharau wakati wa kikao kisha kuamuru afikishwe mahakamani ili akalipe faini hiyo huku akitishia kuwa anaweza kumpiga risasi.
Akizungumzia sakata hilo kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu Kamishna Msaidizi wa Polisi Salum Msangi alikiri kupata malalamiko hayo na kuamuru Kamanda wa Polisi Wilaya ya Maswa Mrakibu wa Polisi (SP) George Salala kulishughulikia kisha kumpa taarifa za madai hayo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment