WALIMU wa sekondari na msingi wa shule zinazomilikiwa na serikali
wilayani Maswa mkoani Simiyu wameonywa kujihusisha na siasa kwani
kufanya hivyo ni kwenda kinyume na taratibu za utumishi wa umma.
Onyo hilo limetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
wilaya ya Maswa, Dk Fredrick Sagamiko wakati akizungumza katika mkutano
mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania( CWT) wa wilaya hiyo ya Maswa.
Alisema kuna wimbi kubwa la watumishi wa Serikali kushiriki masuala
ya vyama vya siasa kwa kasi, huku walimu wakiwa wengi kinyume na Sheria
za Utumishi wa Umma na watakaobainika kwenda kinyume hawataachwa.
Dk Sagamiko amepiga marufuku Idara ya Elimu Msingi na Idara ya Elimu
Sekondari wilayani humo kumhamisha mwalimu bila ya ridhaa ya mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri hiyo.
Katibu wa CWT wilaya ya Maswa, Emanuel Samara alisema walimu wanadai
madeni yao ya muda mrefu ya fedha za likizo na uhamisho na zinapolipwa
wakati mwingine huwa ni pungufu. Chama hicho kimekabidhi mabati 520 ya
Sh milioni 8.8 kwa walimu 26 waliostaafu, ikiwa ni kuwashukuru kwa
utumishi wao uliotukuka.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment