HALMASHAURI ya mji wa Bariadi, Simiyu imesaini mkataba wa Sh bilioni
4.9 na kampuni ya JV Kings & Helem Contractors ya Dar es Salaam
kujenga stendi ya kisasa ya mabasi Somanda na kilomita 1.5 za barabara
ya lami.
Akizungumza kabla ya kusaini mkataba huo, Mkurugenzi wa Halmashauri
ya mji wa Bariadi Melkizedeck Humbe, alisema fedha za mradi huo
zimetolewa kwa mkopo na Benki ya Dunia.
Alisema mradi huo utajumuisha ujenzi wa nyumba na ujenzi wa barabara
hiyo kutoka Bariadi Sekondari hadi Nyamhimbi na barabara ya Ikulu kwenda
ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Alisema mkataba huo utatekelezwa ndani ya mwaka
mmoja na akawataka wakandarasi hao kuzingatia mikataba kuhusu suala la
mazingira.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Bariadi, Robart Lweyo alisema
ujenzi huo utaharakisha maendeleo kwani miundombinu ikikamilika
halmashauri hiyo itapata ushuru wa mabasi.
Lweyo alimtaka mkandarasi huyo kuzingatia muda wa mkataba huo akisema
baadhi ya wakandarasi wanafanya miradi mingi mwisho wake inawashinda
kukamilisha kwa wakati. Mhandisi wa JV Kings & Helem Contractors,
Happy Lebe alisema watajitahidi kutekeleza mradi huo kwa haraka ili
ikiwezekana wakamilishe kabla ya mkataba huo kuisha.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment