Benjamin Sawe
Maelezo
Dar es Salaam
Watu wengi katika jamii yetu ya
Tanzania, ikiwa ni pamoja na baadhi ya viongozi, vijana na watoto hawana uelewa
mzuri kuhusu dhana ya utamaduni. Neno “Utamaduni”
lina uwanda mpana na linaelezwa kwa namna tofauti na watu mbalimbali.
Wataalamu, wanazuoni na wanajamii mbalimbali wametoa maelezo na tafsiri
mbalimbali za dhana ya utamaduni. Tafsiri
hizi tofauti zinatokana na sababu za kijiografia, kihistoria, kimazingira,
kijamii na kipindi au muhula husika.
‘Utamaduni’ ni shughuli au kazi
zote afanyazo mwanadamu na namna anavyokabiliana na mazingira yanayomzunguka
ili kukidhi mahitaji yake muhimu ya kumwezesha kuishi. Mahitaji hayo muhimu ni
Chakula, Makazi na Mavazi. Katika kumwezesha kupata mafanikio aliyotarajia
katika kupata mahitaji hayo, binadamu alijiwekea utaratibu (nguzo) za msingi
katika kutekeleza shughuli zake za kila siku.
Utaratibu (nguzo) huo ulikuwa ni
ule wa kuandaa mazingira ambayo kila mtu alipaswa kuyafuata kila mara anapofanya shughuli zake.
Utaratibu huo ni ule wa kuwa na mila na desturi. Mila na desturi hizi ambazo
mababu zetu wamekuwa wakizifuata kwa miaka mingi ni uridhi ambao tunapaswa
kuuheshimu, kuulinda na kuuendeleza. Kwa maneno mengine, mila na desturi hizo
ambazo ni sehemu ya utamaduni ni rasilimali muhimu sana katika maendeleo ya
taifa letu.
Wahenga walinena ‘mkataa
kwao mtumwa.’ Usemi huu unatufundisha mambo mengi sana ukizingatia mwenendo
wa maisha ya Watanzania katika mazingira ya sasa. Kifupi, usemi huu una maana
kwamba, mtu ambaye anadharau maisha na tamaduni ambazo amekulia nazo, ametekwa kimawazo
na yuko tayari kutumikishwa au kufuata mila na desturi za jamii nyingine
kutokana tu na tofauti ya tamaduni hizo.
Hivi sasa nchi yetu inasura mbili.
Kuna sura ambayo inaonyesha jinsi ambavyo baadhi ya Watanzania baada ya kupata
elimu yao, hususan elimu ya juu ambayo wameipata hapa nchini au nje ya nchi,
wanajiona ni tofauti kabisa na Watanzania wengine. Wasomi hawa wanajiona wako
katika nchi ngeni kabisa na sio ile waliyozaliwa.
Kundi hili linaonekana kudharau
mila na desturi zetu na kuziona kama zimepitwa na wakati. Kundi hili ambalo
linaonekana kuongezeka hapa nchini, linaonekana kutotambua na kutothamini
kabisa utamaduni wetu na mchango wake kwa taifa. Mara nyingi kundi hili
linaonekana likitumia lugha ya kigeni (Kiingereza) zaidi kuliko Kiswahili,
kudhihirisha kuwa ni tofauti na jamii iliyopo.
Kuongea lugha ya Kiswahili kwao
hujiona kama vile hawajaenda shule kabisa. Matokeo haya yanatokana na
mwingiliano wa jamii zetu, kukua na kupanuka kwa nyanja ya mawasiliano na
utandawazi. Aidha, kundi hili linatofautiana kabisa na jamii iliyopo kimavazi,
aina ya chakula wanachokula na aina ya starehe wanazotaka.
Sura ya pili ya nchi yetu ni ile inayotambua
kwamba utamaduni wetu ni muhimu sana katika kuifanya jamii ya kitanzania
kuendelea kufuata mila na desturi katika shughuli mbalimbali za kulijenga taifa
letu.
Jamii hii inalelewa na wazazi
ambao bado wanaamini kuwa utamaduni wetu ni muhimu sana katika kuleta mafanikio
mbalimbali ndani ya jamii. Mfano, nidhamu na kufuata mila na desturi zilizopo
ambazo mababu na bibi zetu wamekuwa wakizifuata na kuweza kuiendeleza amani na
utulivu katika jamii.
Historia ya nchi yetu inaonyesha
kwamba, tangu tupate uhuru, kumekuwepo na amani na utulivu mkubwa katika jamii
zetu. Sababu mojawapo ya msingi ni mshikamano uliokuwepo. Hata hivyo, msingi
mkubwa wa kuwepo na mshikmano huo kulitokana na mawasiliano ambayo yalikuwa
yakifanyika kwa kutumia lugha moja ya Kiswahili.
Licha ya kuwepo na lugha nyingine
za makabila zaidi ya 120, wananchi walikuwa wakitumia zaidi lugha ya Kiswahili kwa
mawasiliano katika shughuli mbalimbali. Kwa maana nyingine, lugha ya Kiswahili
imeweza kuwaunganisha Watanzania wote na kuwa kitu kimoja na hivyo kuwa rahisi
zaidi katika kufuata na kuuendeleza utamaduni katika jamii.
Kama nilivyosema hapo awali
kwamba, Utamaduni ni muunganiko wa mila, imani na desturi ambazo kila jamii
hufuata katika mwenendo wa maisha ya kila siku. Ili kuendeleza utamaduni wetu
tunapaswa kuhakikisha kwamba, masuala ya matumizi ya lugha, mavazi, sanaa na
burudani nk. Ni budi viende sambamba na utamaduni wetu.
Itapendeza zaidi kwa mtu mwenye
uzalendo kuendelea kuheshimu mila na desturi ambazo zinajumuisha matumizi ya
lugha, mavazi, vyakula vya asili, ngoma nk. Mambo haya ndiyo yatamfanya aweze kuwa
tofauti na jamii ya nchi nyingine.
Hata hivyo, pamoja na ukweli
kwamba baadhi ya mila na desturi hizo zimepitwa na wakati, zimesaidia sana
kuilea jamii katika misingi ya utamaduni wetu na kuwa na nidhamu ya hali ya
juu. Jambo la msingi hivi sasa ni kuhakikisha kwamba elimu zaidi inatolewa juu
ya athari inayotokana na baadhi ya mila na desturi hizo potofu na kuendeleza
zile ambazo bado ni msingi imara katika kuendeleza utamaduni wetu na kulijenga
taifa katika misingi ya amani na utulivu.
Ni wazi kwamba, maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano na
kuongezeka kwa utandawazi kumechochea zaidi mabadiliko yaliyopo katika jamii
yetu katika nyanja ya utamaduni. Tofauti zilizopo katika suala zima la kufuata
mila na desturi zinatokana na vijana wengi kujifunza kutoka nchi za kigeni.
Matumizi ya lugha ya Kiingereza
hata pale ambapo kuna ujumbe muhimu kupitia sanaa mbalimbali kama vile muziki,
maigizo, tamthilia nk. inakuwa haina
maana yeyote kwa jamii yetu kwa vile haitambui lugha hiyo. Wakati mwingine
ujumbe kama huo umekuwa ukiposha jamii yetu. Aidha, Matumizi ya mavazi yasiyo
na heshima yamechangia mambo mbalimbali kwa mfano, kuhamasisha vitendo viovu na
vya kihuni kama vile ukahaba ubakaji nk.
Matumizi ya vyakula vya asili yana
faida mbalimbali kwa binadamu katika kujingika na maradhi mbalimbali, kujenga
na kuimarisha virutubisho vya mwili. Matumizi ya vyakula vilivyokaa kwenye
majokofu kwa kipindi karibu wiki mmoja au zaidi vinapoteza radha yake ya asili
na pia hata virutubisho vyenyewe vinapungua au kupoteza kabisa nguvu yake. Aidha
vipo vyakula vilivyozalishwa katika mazingira yasiyo ya asili mfano kuku wa
kisasa vimekuwa vyanzo vikubwa vya matatizo ya kiafya miongoni mwa watu.
Ukifanya uchunguzi wa haraka
haraka utagundua kuwa, wazee wengi ambao wameishi kwa miaka mingi wamekuwa
wakitumia zaidi vyakula vya asili ambavyo vimewasaidia sana katika kuiweka
miili yao katika afya imara. Aidha amani na ututulivu katika jamii imechangia
pia katika kutoa nafasi na uhuru mkubwa wa kufanya mambo mengi ya kimaendeleo
ikiwa ni pamoja na kilimo, ufugaji, uvuvi, na shughuli mbalimbali za
kiutamaduni.
Wakati umefika kwa jamii zetu
kutambua, kuenzi na kuendeleza tamaduni zetu ambazo tumezirithi kutoka kwa
mababu na bibi zetu ili kizazi kipya nacho kiweze kufaidika na tamaduni hizo.
0 comments:
Post a Comment