SERIKALI imesema tangu Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) lianze
utaratibu wa kusahihisha mitihani kwa mashine, umepunguza wasahihishaji
kutoka 3,000 hadi 300. Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya alibainisha hayo wakati akijibu swali
la Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) aliyetaka kufahamu lini
serikali itapeleka bungeni marekebisho ya Sheria ya Necta ili Bunge
kubadili Sheria ya Baraza Kifungu cha 20.
Katika kifungu hicho anataka kuondoa nguvu ya waziri wa Elimu ya
kutoa maelekezo bila kuhoji na kushirikisha wataalamu wa elimu, kama
kubadili aina ya mitihani hasa kuweka maswali ya kuchagua katika soko la
Hisabati.
Alisema utaratibu wa kuchagua kwenye maswali ya Hisabati, umetokana
na sasa utaratibu wa usahihishaji maswali ya mitihani kufanywa na
mashine. Hata hivyo, wanafunzi wanapewa karatasi ya kufanyia mahesabu
kupata majawabu.
Kifungu hicho cha 20 cha Sheria ya Baraza la Mitihani la Taifa,
kinampa mamlaka waziri wa elimu kufanya maamuzi kwa niaba ya serikali,
pale inapolazimika kufanya hivyo kwa kuzingatia mahitaji ya jamii
kulingana na wakati, mazingira halisi na matokeo ya tafiti mbalimbali
kutoka kwa wataalamu pamoja na maoni ya wadau wa elimu.
“Kwa kuzingatia matakwa ya Sheria hii, Baraza la Mitihani Tanzania
hutakiwa kuyatekeleza maamuzi hayo,” alisema Naibu Waziri Manyanya.
Manyanya alisema kwa sasa serikali haina mpango wa kufanyia marekebisho
Kifungu cha 20 cha sheria hiyo kwa kuwa kinamwezesha waziri kufanya
marekebisho mbalimbali kutokana na mahitaji ya jamii yanayojitokeza kwa
wakati husika.
“Waziri hafanyi maamuzi kwa kukurupuka na si kila maamuzi
yanatangazwa mengine hamuyasikii,” alisema. Mbunge wa Segerea, Bonnah
Kaluwa (CCM) katika swali lake la nyongeza alitaka kufahamu lini
serikali itatoa matokeo iliyoyazuia ya wahitimu wa kidato cha nne
walioshindwa kulipa ada, kwani kwa sasa serikali inatoa elimu bure.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa
Joyce Ndalichako alimjibu “Tumelipokea na tutalifanyia kazi na majibu
tutayaleta.”
Chanzo Gazeti la Habari Leo
0 comments:
Post a Comment