Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wananchi wa Kata ya Nkololo
wilayani Bariadi (hawapo pichani) katika Mkutano wa Hadhara, wakati wa ziara yake aliyofanya kwa lengo la
kusikiliza kero mbalimbali za wananchi.
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu na viongozi wengine wa Mkoa na
Wilaya ya Bariadi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) wakati wa
ziara aliyofanya katika Kata ya Nkololo wilayani Bariadi, kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Nkololo wilaya ya Bariadi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka katika Mkutano wa Hadhara aliofanya katika Kata hiyo wakati wa ziara yake yenye
lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi.
Na Stella Kalinga, Simiyu
Wananchi wa Kata ya Nkololo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi wametakiwa
kutambua wajibu wao katika kuchangia ujenzi wa Vyumba vya madarasa ili kupunguza tatizo
la upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule za msingi na sekondari.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka wakati alipokuwa
akijibu kero mbalimbali za wananchi katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Kijiji
cha Nkololo Kata ya Nkololo Wilayani Bariadi.
Mtaka amesema ni vema wananchi wakahamasika kuchangia katika ujenzi wa vyumba vya
madarasa kama wanavyochangia katika masuala mengine ili watoto wao wawe na mazingira
mazuri ya kusomea.
“Kujenga vyumba vya madarasa siyo wajibu wa walimu wetu ni wajibu wenu wenu wazazi,
ni lazima wananchi wa Nkololo mjenge vyumba vya madarasa kama mnavyojitoa katika
mambo mengine, najua hamuwezi kushindwa kutoa angalau mfuko mmoja wa saruji kila
kaya; Nkololo itajengwa na wana Nkololo wenyewe” amesema Mtaka.
Aidha, Mtaka ametoa wito kwa wananchi hao kuzingatia suala la uzazi wa mpango kwa kuwa
ongezeko kubwa la watoto ndio linalopelekea idadi kubwa ya wanafunzi ikilinganishwa na
vyumba vya madarasa.
“Mhe.Diwani nikuombe tengeneza utaratibu hapa na watu wako, Nkololo ni moja ya
centre(kituo) kubwa wachangie, wala wasiseme tumechangia sana ni lazima wachangie; na
kama hatutajirekebisha kwenye kuzaana, tutachanga, tutachanga, tutachanga” amesema
Mtaka.
Naye Afisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Doreen Rutahanamilwa amesema,
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya
elimu vikiwemo vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo, hivyo wananchi wanao wajibu
kuunga mkono jitihada hizo ili kuleta maendeleo katika sekta ya elimu.
Kuhusu kero ya uharibifu wa mazao unaofanywa na wanyamapori hususani Tembo, ambayo
ilitolewa na Luja Masala Mkazi wa Kijiji cha Bubale, Mkuu huyo wa Mkoa amesema,
Serikali kupitia watalaam wake wa Wanyamapori watakabiliana na tatizo hilo, hivyo
akawataka wananchi wasiache kulima na wazingatie ushauri wanaopewa na watalaam hao.
Akitoa ufafanuzi wa kitaalam juu ya kero hiyo, Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili,
Ndg.Mazengo Sabaya amesema, Halmashauri imekuwa ikipeleka askari wa Wanyamapori
katika maeneo yanayovamiwa na tembo na akawataka wananchi kuendelea kufuata ushauri
wa kutumia uzio wa pilipili katika mashamba yao ili kuwazuia tembo hao.
Katika suala la upatikanaji wa mbegu bora, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka
Serikali kupitia kwa wakala wa mbegu ina mpango wa kuhakikisha wakulima wanapata
mbegu bora katika bei wanayoweza kuimudu.
Katika hatua nyingine Mtaka ametoa maelekezo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi
kuhakikisha inaweka mipango ya ujenzi wa stendi, soko na barabara katika kituo cha Nkololo
ambacho ni moja vituo vikubwa vya kibiashara wilayani humo.
Mkuu wa Mkoa ameanza ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi katika Kata ya
Nkololo na baadaye atafanya ziara katika kata za Dutwa na Ngulyati ambapo atafanya
mikutano ya hadhara na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi.
0 comments:
Post a Comment