Posted on: October 4th, 2017
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Eng. Ramo Makani amesema
Wafugaji Nyuki wanayo fursa kubwa ya kujikita katika uanzishwaji wa
viwanda vidogo vidogo vya kuchakata, kufungasha na kuongeza thamani
mazao ya nyuki na kutengeneza vipodozi kutokana na mazao ya nyuki.
Mhandisi Makani ameyasema hayo jana wakati alipozungumza na wafugaji
wa nyuki na wananchi katika Maadhimisho ya Siku ya kutundika Mizinga ya
Nyuki Kitaifa yaliyofanyika katika Kijiji cha Isengwa Wilaya ya Itilima
Mkoani Simiyu, chini ya Kauli Mbiu “UFUGAJI NYUKI KIBIASHARA UNACHANGIA KATIKA UKUAJI WA VIWANDA”
Amesema Mazao ya Nyuki ni malighafi ya Viwanda mbalimbali vikiwemo
viwanda vya vyakula vinavyotumia asali, viwanda vya dawa na vipodozi na
viwanda vya utengenezaji vinavyotumia nta katika kuzalisha maturubai,
dawa za kung’arisha viatu na bidhaa nyingine, hivyo wafugaji wanao
wajibu wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki na ujuzi wa kuyaweka
katika ubora na kuyaongezea thamani.
Aidha, ametoa wito kwa wafugaji wa nyuki kuungana katika vikundi
vyenye usajili ili waweze kuzalisha asali kwa wingi na yenye kufanana,
kwa kuwa ikiwa watazalisha kila mmoja kwa utaratibu wake, asali hiyo
haiwezi kuchanganywa na itakuwa na ubora na sifa tofauti, lakini ikiwa
wataungana na kuzalisha asali nyingi kwa pamoja wakaipima kwa viwango
vya ubora unaotakiwa wataweza kupata soko.
Sanjali na hilo amesema Serikali itahakikisha inawaunganisha wafugaji
nyuki na walaji wa ndani na nje na akabainisha kuwa kwa miaka zaidi ya
11 imekuwa na ushirikiano na soko la Ulaya ambapo sampuli za asali
kutoka maeneo mbalimbali zimepelekwa Ulaya na taarifa za maabara
zinathibitisha kuwa asali ya Tanzania ni salama kwa afya ya mlaji.
Aidha, amesema katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki Serikali
pia inaendelea kutoa elimu kwa wafugaji wa nyuki kuachana na matumizi
ya mizinga ya asili ambayo ni duni na inachukua nafasi kubwa wakati
uzalishaji wake ni mdogo na kuwahamasisha kuanza kutumia mizinga ya
kisasa.
“ Nawaagiza Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki nchini na Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kupitia jukwaa hili, kwamba mbuni
njia rafiki ya kuweka msisitizo katika utoaji wa elimu, uhamasishaji na
kupima mafanikio kila mwaka; taarifa ya utekelezaji wa maagizo haya
itolewe mara kwa mara, taarifa ya kwanza baada ya agizo hili itolewe
katika siku ya maadhimisho kama haya mwaka kesho 2018” aliagiza Naibu
Waziri
Katika hatua nyingine Mhe. Makani amepongeza juhudi zinazofanywa na
Mradi wa LVEMP II katika kuboresha mazingira na kubainisha kuwa pamoja
na kuhifadhi rasilimali za asili za Bonde la Ziwa Victoria ambayo
husaidia kutunza vyanzo vya maji na mazingira hayo yanafanywa kuwa
mazingira bora kwa ufugaji nyuki, ambapo katika wilaya ya Itilima kuna
vikundi 22 vyenye mizinga 2080 ya nyuki vinavyofadhiliwa na LVEMP.
Akitoa salamu za Mkoa kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu,
Ndg.Chele Ndaki amesema idadi ya wafugaji na mizinga ya nyuki imekuwa
ikiongezeka kila mwaka ambapo kwa sasa kuna jumla ya vikundi 91 vyenye
jumla ya mizinga 5824 na akaahidi kuwa mkoa utaendelea kusimamia
uboreshaji wa mazingira ya ufugaji nyuki na kusimamia vikundi
vinavyoanzishwa katika Halmashauri., ili wafugaji wanufaike na
kujiimarisha kiuchumi
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania(TFS) Ndg.Herberth Haule amesema shughuli ya ufugaji wa
nyuki inasaidia katika uhifadhi wa mazingira na kujenga uchumi kwa
wananchi hususani vikundi vinavyojishughulisha na kazi hiyo.
Naye Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki kutoka Wizara ya Maliasili na
Utalii, Dkt.Ezekiel Mwakalukwa amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi
Tano za Afrika zinazoruhusiwa kuuza asali yake katika soko la Ulaya na
nchi ya China
Nao wafugaji wa nyuki na wajasiriamali wa mazao ya nyuki wameiomba
Serikali pamoja na wadau wengine kuwekeza katika viwanda vya kutengeneza
vifungashio kwa kuwa suala hilo ni changamoto kwao ambayo inawalazimu
kuagiza vifungashio nje ya nchi kwa kutumia gharama kubwa.
Maadhimisho ya Siku ya Kutundika Mizinga ya Nyuki Kitaifa kwa mwaka
2017 yameadhimishwa kwa mara kwanza Mkoani Simiyu yakiwa ni maadhimisho
ya tano kufanyika hapa nchini, ambapo kwa mara ya kwanza yalifanyika
mwaka 2013 Mkoani Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(kushoto) akimsikiliza Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Eng.Ramo Makani(Mb) (kulia) kabla ya
kuanza safari kuelekea kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kutundika Mizinga
ya Nyuki Kitaifa yaliyofanyika katika Kijiji cha Isengwa Wilaya ya
Itilima Mkoani humo.
Kutoka kulia Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe.Dkt. Titus Kamani,
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Eng.Ramo Makani(Mb) na Mkuu wa
Wilaya ya Itilima, Mhe.Benson Kilangi wakizungumza jambo, wakati wa
Maadhimisho ya siku ya kutundika Mizinga ya Nyuki Kitaifa yaliyofanyika
jana katika Kijiji cha Isengwa Wilayani Itilima katika Mkoa Simiyu.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Eng.Ramo Makani(Mb) (mwenye
skafu) akiangalia mazao ya Nyuki alipotembelea Banda la maonesho la
Kikundi cha Wafugaji Nyuki cha Malela wilayani Itilima, wakati wa
Maadhimisho ya siku ya kutundika Mizinga ya Nyuki Kitaifa yaliyofanyika
jana katika Kijiji cha Isengwa Wilayani humo katika Mkoa Simiyu.
Mbunge wa Jimbo la Itilima Mhe.Njalu Silanga akizungumza wakati wa
Maadhimisho ya siku ya kutundika Mizinga ya Nyuki Kitaifa yaliyofanyika
jana katika Kijiji cha Isengwa Wilayani Itilima katika Mkoa Simiyu.
Chanzo Tovuti ya Mkoa wa Simiyu
0 comments:
Post a Comment