Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King akisisitiza
jambo wakati wa ziara ya Kamati ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mnara
wa TTCL kwenye kijiji cha Sanga Itinje kilichopo Kata ya Itinje wilaya
ya Meatu mkoani Simiyu. Kushoto kwa Mwenyekiti ni Mtendaji Mkuu wa Mfuko
wa Mawasiliano kwa Wote Eng. Peter Ulanga.
Mkuu
wa Mkoa wa Mwanza Bwana John Mongella akiongea kuhusu mchango wa mifumo
ya mawasiliano katika kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali
mbele ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu na watendaji wa kampuni za simu
wa mkoani Mwanza (hawapo pichani) wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya
kukagua ujenzi wa minara, ufikishaji na upatikanaji wa huduma za
mawasiliano vijijini mkoani Mwanza. Aliyeketi ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King.
Meneja
wa TTCL mkoa wa Shinyanga Bwana Abdallah Lugage akitoa taarifa kwa
Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mnara wa
kampuni hiyo kwenye kijiji cha Sanga Intinje kilichopo kata ya Intinje
wilaya ya Meatu mkoani Simiyu. Wa tatu kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati
hiyo Prof. Norman Sigalla King.
Wajumbe
wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, watendaji wa Mfuko wa Mawasiliano
kwa Wote, wafanyakazi wa TTCL na wanakijiji wakiwa kwenye picha ya
pamoja wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa
mnara wa kampuni hiyo kwenye kijiji cha Sanga Intinje kata ya Intinje
iliyopo wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.
Serikali
ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na
Dkt. John Pombe Magufuli imesisitiza kwa taasisi za Serikali, sekta
binafsi na wananchi kwa ujumla kulipa kodi kwa wakati ili nchi iweze
kuongeza mapato yake kwa lengo la kukuza uchumi, kujenga miundombinu ya
barabara, reli, bandari, mawasiliano, kuboresha utoaji wa huduma za
kijamii na kuweza kuwatumika wananchi.
Hayo
yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Prof.
Norman Sigalla wakati wa ziara ya Kamati yake ya kukagua ujenzi wa
minara, ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini na
kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa kibishara kwenye mikoa ya kanda ya ziwa
ya Mwanza na Mara ambapo Serikali imetoa ruzuku kwa makampuni ya simu
za mkononi ili ziweze kutoa huduma za mawasiliano kwa wananchi kupitia
Mfuko wa Mawasiliao kwa Wote (UCSAF) ulio chini ya Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano.
Ameongeza
kuwa Kamati yake inasimamia sekta ya miundombinu yote nchini ikiwa ni
pamoja na miundombinu ya mawasiliano ambayo inategemewa na Serikali
katika kukuza uchumi na kuiwezesha nchi yetu kufikia uchumi wa kati na
kuwa nchi ya viwanda. Prof. Norman Sigalla King amesema kuwa miundombinu
na huduma za mawasiliano ni moja ya nguzo kuu za ukuaji wa uchumi,
inachochea maendeleo ya taifa letu na kuiwezesha Serikali kuhudumia
wananchi wake kwa haraka, wakati, kwa ufanisi na kupunguza gharama za
Serikali kuwahudumia wananchi na kuokoa muda. “Serikali imepeleka fedha
nyingi kwa ajili ya miundombinu mbalimbali ya nchi yetu kupitia Wizara
hii kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2017/2018 ili nchi
iweze kusonga mbele”, amesema Prof. Norman Sigalla King.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bwana John Mongela ameieleza Kamati hiyo kuwa
mifumo ya mawasiliano imeiwezesha Serikali ya Mkoa wake kuongeza
makusanyo ya mapato katika Halmashauri za mkoa huo kutoka chini ya
asilimia 46 kwa mwaka wa fedha uliopita na kufikia asilimia 70 kwa mwaka
huu wa fedha ambapo Halmashauri hizo zinatumia zaidi ya asilimia 70 ya
makusanyo hayo kuendesha miradi ya maendeleo na kutekeleza majukumu
mengine ya mkoa.
“Suala
la mawasiliano duniani popote pale ni nyeti sana kwa kuwa shughuli zote
zinafanywa na mawasiliano kama vile miamala ya kifedha, ulinzi na
usalama wa raia na mali zake ambapo katika ngazi ya Mkoa tumedhibiti kwa
kiwango kikubwa ulinzi na usalama wa raia wetu na hali ya mawasiliano
kwenye mkoa wetu ni nzuri na tuna Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano,”
amesema Mongella. Ameongeza kuwa Mkoa huu ni mkoa wa pili kwa ukubwa wa
idadi ya watu na ni mkoa wa pili ambao unaongoza kwa kuchangia kwa kiasi
kikubwa mapato na ukuaji wa uchumi wa taifa letu.
Naye
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Eng. Peter Ulanga
amesema kuwa Mfuko umetoa ruzuku kwa kampuni za simu za mkononi ili
kufikisha huduma za mawasiliano kwenye mikoa ya kanda ya ziwa na visiwa
vyake takribani 36 vilivyopo kwenye kanda hii ili waweze kutumia
mawasiliano kwa ajili ya ulinzi na usalama na shughuli nyingine za
kiuchumi na kijamii.
Ameongeza
kuwa kupitia Halotel, UCSAF imepeleka mawasiliano kwenye vijiji 78
vilivyopo kanda ya ziwa na ziara hii inatusaidia kupata maoni ya wadau
na kukusanya changamoto ambazo zitasaidia kuboresha jukumu la UCSAF la
kufikisha huduma za mawasiliano vijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa
kibiashara nchini nzima.
Mtaalamu
wa miundombinu wa kampuni ya simu ya Halotel wa Mkoa wa Mwanza na
Simiyu Bwana Emmanuel Masanja amesema kuwa kampuni yao inajenga minara
kwa kukodisha au kupewa ardhi na mamlaka za serikali za vijiji kwa ajili
ya ujenzi wa minara hivyo wanaishukuru Serikali kuwapatia ruzuku ya
kufikisha mawasiliano vijijini.
Ameongeza
kuwa baadhi wa watu wanazuia maendeleo ya ujenzi wa minara kwenye
baadhi ya maeneo vijijini ambapo yanasababisha migogoro ambayo inachukua
muda mrefu kukamilishwa hivyo kuchelewesha ujenzi wa minara na
ufikishaji wa huduma za mawasiliano vijijini.
Bwana
Masanja amesema kuwa kampuni yao wanaiomba Serikali iwasaidie kusimamia
upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa minara ya mawasiliano kwenye
ngazi ya Halmashauri zote nchi nzima ili kuwawezesha wakandarasi
kujenga minara kwa wakati ili kuharakisha jitahada za Serikali ya Awamu
ya Tano Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufikisha huduma za mawasiliano
kwenye vijiji vyote nchi nzima na maeneo yasiyokuwa na mvuto wa
kibiashara.
Aidha
Mkurugenzi wa Kanda ya Ziwa wa kampuni ya TIGO Bwana Ally Maswanya
ameishukuru Serikali kwa kuwapatia ruzuku ya kujenga minara na kufikisha
huduma za mawasiliano vijijini kwa kuwa kampuni zetu zinafanya biashara
hivyo haikuwa rahisi kwa kampuni za simu za mkononi kuwekeza bali UCSAF
imetuwezesha kusambaza mawasiliano vijijini. Vile vile ameiomba
Serikali kuwasaidia kufikisha umeme kwenye minara kupitia Wakala wa
Nishati ya Umeme Vijijini (REA) kwa kuwa inawapa changamoto ya kuongeza
gharama za kuendesha minara hiyo na umeme wa jua hautoshelezi.
Ameongeza
kuwa sisi kama kampuni ya Halotel tunapata ushirikiano mkubwa kutoka
ofisi za Wakuu wa Mikoa na wilaya kwenye maeneo mbalimbali nchini kwa
ajili ya kujenga minara bali changamoto ipo kwenye ngazi za Halmashauri
za upatikanaji wa ardhi na utatuzi wa migogoro ya ardhi na ukosefu wa
ushirikiano wa kutosha kutoka kwa mamlaka husika ili kufanikisha
ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini.
Mwenyekiti
Prof. Sigalla amesema kuwa nguzo za uchumi mojawapo ni miundombinu kwa
maana ya barabara, bandari, reli na mawasiliano na ndiyo maana serikali
imepeleka fedha nyingi kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/18.
Ametoa rai kwa wananchi kuwa watoe ulinzi kwenye minara yote ya
mawasiliano nchini kwa kuwa Serikali inatumia kodi za wananchi kujenga
minara.
Ameongeza
kuwa wananchi watumie fursa ya mawasiliano kwa maendeleo na kujenga
uchumi wao na maendeleo ya taifa. Pia ameyaomba makampuni ya simu yote
nchini ambayo yamepatiwa ardhi na serikali ya kijiji na kujenga minara
irudishe faida kwa wananchi wa eneo husika kwa kuwapatia fedha au huduma
za kijamii.
Amesisitiza
kuwa kampuni za mawasiliano zitumie fedha waliyopewa na Serikali
kujenga minara na kufikisha huduma za mawasiliano vijijini kwa wakati
kwa kuwa ucheleweshaji wa kutekeleza jukumu hilo unawanyima wananchi
haki ya kupata huduma za mawasiliano. Pia ameongeza kuwa kwa namna yoyte
ile kampuni haziwezi kulipa gharama za ucheleweshaji wa kujenga minara
hiyo na upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi na Serikali
kwa ujumla. “Maendeleo ni vita, ukipewa ruzuku na Serikali ya kujenga
minara na ukichelewesha ni hasara; hakikisheni mnakimbizana kukamilisha
jukumu hilo kwa wakati,” amesema Prof. Norman Sigalla King.
Aidha,
ametoa rai kwa kampuni za simu zinazopatiwa ardhi bure na Serikali za
vijiji mbalimbali nchini kote kutoa fedha kwa vijiji hivyo sehemu ya
fedha wanazopata ili vijiji viweze kunufaika na uwepo wa minara hiyo kwa
kuwa kampuni zinafanya biashara.
Ametanabaisha
kuwa minara haina madhara kwa wananchi ukilinganisha na usikilizaji wa
simu za mkononi kwa muda mrefu zaidi ya dakika tisa. Amewatahadhirisha
wananchi kuwa wananchi wasikilize simu kwa muda mfupi na isizidi dakika
tisa.
“wananchi
watumie vifaa vya kusikiliza simu masikioni kwa wale ambao wanasikiliza
simu kwa muda mrefu na minara inayowekwa na UCSAF ni salama na tumieni
simu kwa maendeleo chanya,” amesema Prof. Norman Sigalla King. Pia
ameipongeza Wizara kwa kazi kubwa inayofanya ya kujenga na kusimamia
miundombinu iliyopo kwenye sekta ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
0 comments:
Post a Comment