Home » » Atiwa mbaroni akidaiwa kuua shemeji zake wawili kwa kisu

Atiwa mbaroni akidaiwa kuua shemeji zake wawili kwa kisu



 
Na Mwandishi wetu
Masasila Masolwa, mkazi wa Kijiji cha Shininga katika Kata ya Kilago wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuwaua shemeji zake wawili kwa kuwachoma visu.
Diwani wa Kata ya Kilago, Peter Emmnuel, alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 4:00 usiku baada ya kutokea mabishano kati mke wa mtuhumiwa, Fatuma Suleimani na shemeji zake.
Alisema kuwa mabishano hayo yalitokana na mke wa mtuhumiwa aliyekuwa amelima bustani pembeni ya nyumba yake kuwatuhumu wake wa shemeji zake kuwa wanachuma mboga zake nyakati za usiku.
Alisema kuwa baada ya mke wa mtuhumiwa kubaini hivyo alikwenda kushitaki kwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Shininga, John Ikombe.
Alisema baadaye Masolwa alichukua kisu na kuanza kuwashambulia shemeji zake hao wawili January Selemani (30) na Emmnuely Selemani (25), hali iliyopelekea kuvuja damu nyingi kutokana na majeraha makubwa na kufariki dunia papo hapo.
Mtuhumiwa huyo baada ya kubaini kuwa amefanya mauaji, aliamua kutorokea kwa mganga wa kienyeji, lakini baada ya wananchi kupeana taarifa walifanikiwa kumkamata akiwa kwa mganga wa kienyeji ambaye jina lake halikuweza kufahamika.
Jeshi la Polisi wilayani Kahama limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa linamshikilia Masolwa pamoja na mganga wa kienyeji na kuongeza kuwa litawafikisha mahakamani upelelezi utakapokamilika.
CHANZO: NIPASHE
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa