KUELEKEA MTIHANI WA TAIFA MEI 2018 WANAFUNZI 1003 KIDATO CHA SITA SIMIYU WAPIGA KAMBI YA KITAALUMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wanafunz wa Kidato cha Sita kutoka shule 11 za Mkoa huo wakati wa ufunguzi wa Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi hao Aprili 03 wilayani Maswa.
Baadhi ya Wanafunzi wa Kidato cha Sita kutoka shule 11 za Mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi hao Aprili 03 wilayani Maswa.
Baadhi ya walimu mahiri 40 waliochaguliwa kufundisha na kuwaandaa wanafunzi wa kidato cha sita (kutoka shule 11 mkoani Simiyu) na Mtihani wa Taifa utakaofanyika mwezi Mei mwaka huu, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa Kambi ya  Kitaaluma kwa wanafunzi hao Aprili 03 wilayani Maswa.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe.Dkt.Seif Shekalaghe akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita kutoka shule 11 za Mkoa wa Simiyu wakati wa ufunguzi wa Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi hao Aprili 03 wilayani humo. 
Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl.Julius Nestory akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita kutoka shule 11 za Mkoa huo wakati wa ufunguzi wa Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi hao Aprili 03 wilayani Maswa.




Na Stella Kalinga, Simiyu

Takribani wanafunzi 1003 wa Kidato cha sita kutoka shule za Sekondri 11 zenye kidato cha tano na sita Mkoani Simiyu, wamepiga kambi katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa na Shule ya Sekondari Binza, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Mtihani wa Taifa ambao unatarajia kufanyika mapema mwezi Mei mwaka huu.

Akifungua kambi hiyo Aprili 03 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa wilayani Maswa, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema ili mkoa huo uweze kushindana na kufanya mageuzi katika Uchumi ni lazima kuwekeza katika elimu.

“Kama wanafunzi wetu wanakaa makambi ya michezo ngazi ya kata, wilaya, mkoa na Taifa kwa nini wanafunzi hao hao wasikae kambi kwa ajili ya maendeleo ya taaluma; tukitaka kufanya mageuzi ya Mkoa huu ni lazima tuweke nguvu kwenye elimu, maeneo yenye uchumi mzuri wamewekeza sana  kwenye elimu” alisema Mtaka. Aidha, Mtaka awataka wanafunzi wote wa kidato cha sita kuwasikiliza walimu watakaokuwa wakiwafundisha na kuwaelekeza na akawataka kujiamini wakati wa mtihani wao wa mwisho.

Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Mwl. Julius Nestory amesema Mkoa huo una mpango wa kuondoa daraja la nne na sifuri katika matokeo ya Mitihani ya Taifa, hivyo wanayo matumaini makubwa kuwa, kupitia makambi hayo ya kitaaluma Mkoa utaweza kufikia lengo hilo kwa matokeo ya kidato cha sita mwaka 2018.

“ Tumeamua kuwaleta pamoja wanafunzi ili waweze kunyanyuka kama kundi moja la mama mmoja (Simiyu) na kuweza kupandisha ufaulu, tumewaleta hapa ili kuweza kunyanyua morali wa kazi kuwaleta pamoja anayeweza na asiyeweza ili tuweze kunyanyuka pamoja kama kundi” alisema Mwl.Nestory.

Amesema katika siku 10 za kambi wanafunzi wa kidato cha sita watapitishwa katika miiko ya watahiniwa wakati wa mitihani kwa kuwa mkoa wa Simiyu unapinga suala la udanganyifu kwenye mitihani, watapitishwa katika maswali na mada ambazo baada ya tathmini ilionekana hawakufanya vizuri katika mtihani wa kanda na mtihani wa Mkoa.

Akizungumza kwa niaba ya walimu mahiri 40 ambao watakuwa wakiwafundisha na kuwasaidia wanafunzi hao, Mwl.Majaliwa Chibona wa Shule ya Sekondari Mwandoya wilayani Meatu amesema, wamejipanga kuwasaidia wanafunzi katika kuwapa mbinu na mikakati mbalimbali itakayowasaidia kujiandaa na mitihani wao wa mwisho ili waweze kufaulu.

Nao baadhi ya wanafunzi wamesema kambi hiyo itawasaidia sana katika kuwajengea hali ya kujiamini kwa kuwa watasaidiwa na walimu katika maeneo yote yanayoonekana magumu kwao, watasaidiana wa kwa wao kupitia makundi na watapewa mbinu zitakazowasaidia kujiandaa vema na hatimaye kufanya vizuri.

WAZIRI KABUDI AWATAKA WASAJILI WA VYETI VYA KUZALIWA MIKOA YA SIMIYU, MARA KUZINGATIA UMAKINI NA UZALENDO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi(wa tatu kushoto) akizindua Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara, katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (katikati) akionesha nakala ya cheti cha kuzaliwa kinachotolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri huo na kutoa vyeti vya kuzaliwa, kwa mikoa ya Simiyu na Mara uliofanyika Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akimkabidhi mkazi wa Manispaa ya Musoma cheti cha kuzaliwa cha mtoto wake mwenye umri wa chini ya miaka mitano, mara baada ya uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa, kwa mikoa ya Simiyu na Mara, uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini hapa nchini (RITA), Bi. Emmy Hudson akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara, uliofanyika Uwanja wa Shule ya msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akitoa salama za Mkoa wa Simiyu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka, wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara, katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Wasanii wa Kikundi cha Ngoma ya Asili cha Wagoyangi kutoka Maswa mkoani Simiyu wakitoa burudani wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara, katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (katikati kwa walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mikoa ya Simiyu na Mara mara baada ya uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa hiyo uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma.
Na Stella Kalinga, Simiyu

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Prof. Palamagamba Kabudi amewataka wasajili wa vyeti vya kuzaliwa kupitia mpango wa usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kwenye mikoa ya Simiyu na Mara, kufanya kazi hiyo kwa umakini na uzalendo mkubwa katika kuhakikisha wanawasajili watoto wenye sifa.

Waziri Kabudi ametoa rai hiyo Machi 20 wakati wa Uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa, katika mikoa ya Simiyu na Mara uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.

“Mikoa ya Mara na Simiyu ina muingiliano mkubwa sana na wananchi wa nchi jirani hivyo wasajili wawe makini na watangulize uzalendo wakati wa kutekeleza mpango huu, tusisajili mtoto ambaye hahusiki na pale ambapo tuna mashaka kuwa mtoto huyo anaweza kuwa wa nchi za jirani, tutoe taarifa kwa vyombo vinavyohusika ili hatua za kiusalama zichukuliwe” alisema Profesa Kabudi.

Amesema kuwa usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano unafanyika bila malipo hivyo wasajili wasitumie kwa namna yoyote mpango huo kama fursa ya kujipatia fedha kwa udanganyifu.Aidha, Waziri Kabudi ameahidi kutoa tuzo maalum kwa mkoa (kati ya Simiyu na Mara) utakaofikia asilimia 80 ya lengo la usajili kwa kipindi cha miezi miwili tangu usajili ulipoanza na wakati huo huo akawataka Viongozi wa Taasisi zote Umma kuvitambua vyeti vitakavyotolewa chini ya mpango huo kwa kuwa ni vyeti halali

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini hapa nchini (RITA) Profe. Hamis Dihenga amesema kupitia mpango wa usajili na kutoa vyeti kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, RITA inakusudia kusajili jumla ya watoto 735, 545 katika mikoa ya Simiyu na Mara kwenye vituo 463 (Mara) na Vituo 324 (Simiyu).

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mhe.Annarose Nyamubi akiwasilisha taarifa ya Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe.Adam Malima amesema hadi sasa Mkoa huo umesajili jumla ya watoto 78, 625 na watahakikisha watoto wote wanaopaswa kusajiliwa wanasajiliwa ndani ya miezi miwili na baadaye kuendelea na usajili kwa watoto watakaozaliwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga, akitoa salamu za Mkoa wa Simiyu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka amesisitiza wananchi kutambua umuhimu wa kuwasajili watoto wao ili waweze kutambulika, kupewa vyeti vya kuzaliwa na Serikali iweze kupata takwimu sahihi.

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Watoto (UNICEF) hapa nchini ambao ni miongoni mwa wafadhili wa mpango huu, Bi. Maud Droogleever , amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano wanasajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.

Baadhi ya wananchi wa Mikoa ya Simiyu na Mara walioshirikia katika Uzinduzi wa Mpango huo wameishukuru Serikali kwa kuleta mpango huo kwa kuwa umewarahisishia huduma ya kupata vyeti vya kuzaliwa kwa kuwasogezea huduma hiyo katika Ofisi za kata tofauti na ilivyokuwa awali ambapo walikuwa wanalazimika kufuata huduma hiyo katika Ofisi za Wakuu wa Wilaya
 

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE UTAWALA NA SERIKALI ZA MITAA YAVUTIWA NA MIRADI YA TASAF MKOANI SIMIYU.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399

Wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakiwa mbele ya nyumba iliyojengwa na mmoja wa Walengwa kwa ruzuku ya TASAF Bi. Monica Mwalu, (aliyekamata karatasi) katika kijiji cha Shanwa wilayani Maswa . Aliyevaa kofia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika.
Mmoja wa wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ,Mhe. Venance Mwamoto (aliyevaa koti) akitoka ndani ya nyumba iliyojengwa na mmoja wa walengwa kwa ruzuku ya TASAF.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa , Wakikagua moja ya Majengo yaliyojengwa na TASAF katika shule ya Sekondari ya Nyalikulungu katika wilaya ya Maswa mkoani Simiyu.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya Nyalikulungu wilayani Maswa wakisikiliza hotuba ya Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe.Steven Rweikiza (hayupo pichani).
Baadhi ya Walengwa wa TASAF katika kijiji cha Shanwa wilaya ya Maswa wakisikiliza hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Rweikiza( hayupo pichani) wakati kamati hiyo ilipokagua miradi ya TASAF mkoani Simiyu.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa , wakimsikiliza mmoja wa Walengwa wa TASAF Bi.Monica Mwalu mkazi wa kijiji cha Shanwa wilayani Maswa namna alivyotumia sehemu ya ruzuku kujiongezea kipato na kujenga nyumba (iliyoko nyuma yao) kuboresha makazi yake.
Waziri Mkuchika (aliyevaa kofia ) na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakikagua zoezi la ilipaji wa ruzuku kwa Walengwa wa TASAF katika kijiji cha Shanwa Wilayani Maswa ruzuku ambayo imeanza kuboresha maisha yao kwa kiwango kikubwa. 
NA ESTOM SANGA- BARIADI

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wamefanya ziara mkoani Simiyu na kuvutiwa na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF-mkoani humo.

Wajumbe hao walianza ziara yao kwa kusomewa taarifa ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ambapo Katibu Tawala wa Mkoa huo , Jumanne Sagini aliwajulisha Wajumbe hao kuwa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na TASAF,umekuwa chachu muhimu katika kuleta maendeleo ya wananchi katika mkoa huo mpya.

Amesema kupitia Mpango huo Walengwa wameboresha maisha kwa kuendelea kujenga mkazi bora, kuchimba visima vya maji, uanzishwaji wa mashamba ya pamba ili kujiongezea kipato huku pia sekta za Afya na Elimu zikiendelea kunufaika na utekelezwaji wa Miradi ya TASAF.

Wakiwa katika Wilaya ya Maswa ,mkoani humo, Wajumbe hao walioongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.Dkt Jasson Samson Rweikiza, walipata fursa ya kutembelea baadhi ya kaya za Walengwa ambako walishuhudia mafanikio ya ujenzi wa Nyumba ya mmoja wa Walengwa wa TASAF ,Monica Kwilasa katika kijiji cha Shanwa ambaye ametumia sehemu ya ruzuku aliyopata kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kuboresha Makazi yake.

Kama Wahenga wasemavyo “ Kuona ni kuamini” Wajumbe wa kamati hiyo walionyesha kushangazwa na mafanikio ya Mlengwa huyo ambaye aliwajulisha namna alivyotumia fedha alizozipata kutoka TASAF kuanzisha biashara ndogo ndogo iliyomwongezea kipato na kumwezesha kujenga nyumba kwa matofali ya saruji na kuezeka kwa mabati.

Akizungumza na Walengwa na Wananchi katika eneo la shule ya Sekondari ya Nyalikulungu ambako pia TASAF imejenga majengo, Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Rweikiza,amesema mafanikio yaliyoanza kupatikana katika utekelezaji wa Mpango huo ni kielelezo cha namna Serikali inavyopiga vita umaskini kwa kutumia mbinu mbalimbali ambazo amesema zinapaswa kuungwa mkono na wananchi. Zifuatazo ni picha za ziara hiyo ya kamati ya huduma za jamii ya bunge. 

BIL.1.7 KUJENGA MIUNDOMBINU YA ELIMU SIMIYU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mheshimiwa Anthony Mtaka akimuelezea Makamu wa Raisi utekelezaji wa mpango wa EQUIP-Tanzania mkoani Simiyu.
Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza nchini Tanzania Bibi Elizabeth Arthy akizungumza mbele ya makamu wa Rais juu ya mchango wa serikali ya Uingereza katika kuboresha elimu.
Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza nchini Tanzania Bibi Elizabeth Arthy akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa shule ya msingi Gamondo A iliyoo wilayani Bariadi mkoani Simiyu.
Bibi Elizabeth Arthy alipotembelea shule ya msingi Gamondo A mkoani Simyu, kuona utekelezaji wa mpango wa EQUIP-Tanzania.
 
Uwekezaji katika sekta ya elimu Nchini kupitia mpango wa kuinua ubora wa elimu (EQUIP-Tanzania) ambao umelenga kuboresha mchakato wa kufundisha na matokeo ya kujifunza kwa watoto nchini umeweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa Mkoani Simiyu.

Uwekezaji huo ambao unafadhiliwa na serikali ya Uingereza kupitia Wizara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza (DFID) umeleta ufanisi wa elimu na kufanya viwango cha ufaulu kuwa juu kutoka asilimia 36 mwaka 2013 mpaka asilimia 68 2017.

Na katika kutimiza hayo Jumla ya kiasi cha shilingi Bil 1.7 kutoka DFID kupitia mradi wa kuinua ubora wa Elimu Nchini (Equip) zimetolewa kwa Serikali ya Mkoani Simiyu kwa ajili ya kujenga na kuboresha miundombinu ya elimu Mkoani humo .

Akizungumzia nia ya serikali ya Uingereza wakati wa mazungumzo na Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan , Mkuu wa DFID-Tanzania Elizabeth Arthy alisema wametoa kiasi hicho cha fedha kwa serikali ya Mkoa wa Simiyu ili kuhakikisha wanatatua changamoto ya miundombinu iliyopo.

Arthy alisema kuwa kiasi hicho cha fedha ambacho kinatarajiwa kutumika katika kuboresha miundombinu hiyo na kujenga vyumba vya madarasa, ofisi za walimu pamoja matundu ya vyoo kitasaidia kwa kiasi kikubwa kuleta ufanisi wa utoaji elimu kwa walimu na wanafunzi.

Mkuu huyo alieleza kuwa tangu shirika lake lianze kusaidia katika Elimu ,Mkoa wa Simiyu umeweza kupata mafanikio makubwa na ya haraka ambayo yamesaidia kuuweka Mkoa katika nafasi nzuri Kitaifa katika matokeo ya mitihani ya kuhitimu elimu ya Msingi.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka aliuelezea mpango wa kuinua ubora wa elimu Tanzania kwa Mkoa wake kuwa ni mpango ambao umeweza kuleta mabadiliko makubwa ya kukuza viwango vya ufaulu wa wanafunzi.

Mtaka anaeleza wanalishukuru shirika la maendeleo ya uingereza (DFID) kupitia mpango wa kuinua ubora wa elimu kwa kuona kuwa Tanzania na Mkoa wake unahitaji msaada huo wa kuinua kiwango cha ufaulu pamoja na uboreshaji wa mazingira ya elimu.

Amesema kupitia msaada huo wa fedha kiasi cha shilingi Bil 1.7 zilizotolewa kwao na shirika la DFID kwa mwaka huu za kuboresha mazingira ya elimu ,zitawasaidia kujenga vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo ambavyo vyote hivyo ni changamoto kubwa Mkoani kwake.

Anaongeza kuwa kupitia fedha hizo anaanimi tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo utapungua kwa kiasi kikubwa na kwamba atasimamia vema fedha hizo ili ziweze kutumika ipasavyo.
 

MAKAMU WA RAIS AHUDHURIA MAHAFALI YA 34 YA CHUO KIKUU HURIA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akishiriki matembezi ya mahafali ya 34 ya Chuko Kikuu Huria pamoja na Mkuu wa chuo hicho Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda (kulia) kuelekea kwenye uwanja wa Halmashauri ya  Bariadi kwenye sherehe za mahafali ya 34 ya Chuo Kikuu Huria Tanzania. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais) 
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Huria Tanzania Profesa Rwekaza Mukandala wakati wa mahafali ya 34 ya chuo hicho yaliyofanyika kwenye uwanja wa Halmashauri ya Bariadi mkoani Simiyu. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

 Sehemu ya Wanafunzi waliohitimu katika Chuo Kikuu Huria wakiwa kwenye sherehe za mahafali ya 34 ya chuo hicho. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

MAKAMU WA RAIS AANZA ZIARA MKONI SIMIYU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa maji Kiloleli ambao utafaidisha vijiji vitatu, kulia ni Mbunge wa Jimbo la Busega Dkt. Raphael Chegeni.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasalimia wananchi wa Masanza Kona, Kiloleli wilaya ya Busega mkoani Simiyu.
Mbunge wa Jimbo la Busega Dkt. Raphaele Chegeni akizungumza mbele ya Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa kusalimia wananchi waliojitokeza kwa wingi barabarani eneo la Nyashimo kumsalimia Makamu wa Rais ambaye ameanza ziara ya siku tano mkoani Simiyu.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba za Viongozi wa Mkoa katika eneo la Nyaumata, kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi wa mkoa wa Simiyu kuhakikisha kila shule ya sekondari inayojengwa inajengwa ikiwa na maabara.

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati akiwahutubia wananchi Lamadi wilaya ya Busega mkoani Simiyu ikiwa siku yake ya kwanza ya ziara ya siku tano mkoani humo.

Makamu wa Rais ambaye alianza ziara yake kwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa maji uliopo Kiloleli ambapo mradi huo ukikamilika utasaidia kupatikana kwa maji safi na salama kwa vijiji vitatu na utagharimu shilingi za kitanzania bilioni 1.6 ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 80%.

Makamu wa Rais aliwapongeza wananchi kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano katika uwekezaji na uendelezaji wa viwa nda ambapo mpaka sasa kuna viwanda 14 vya usindikaji wa pamba na viwanda vidogo vidogo vya usindikaji mazao 1,035.

“Nawapongeza kwa mkakati wa kuzalisha bidhaa za afya zinazotokana na pamba na maji ya drip”

Makamu wa Rais aliwaambia wananchi hao kuwa hadi mwisho wa mwezi huu chupa milioni 2 za dawa za kuuwa wadudu wanaoshambulia pamba zitakuwa zimesambazwa.

Mwisho Makamu wa Rais aliwataka Viongozi na Watendaji kushirikiana na wananchi kwani ushirikiano


Katiak Ziara hiyo Makamu wa Rais aliweka pia jiwe la msingi la ujenzi wa Nyumba za Viongozi wa Serikali zilizopo Nyaumata.

MAMBO TISA YA KUFANYA KUITANGAZA BIASHARA YAKO MSIMU HUU WA SIKUKUU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Na Jumia Travel Tanzania

Kipindi cha sikukuu na mapumziko ya mwisho wa mwaka huongoza kwa watu kufanya manunuzi ya aina mbalimbali. Ni kipindi ambacho si watu hujikita zaidi kwenye kufurahia likizo zao bali hata kuwa huru kutumia pesa kwa ajili ya chakula, zawadi na huduma kadha wa kadha.
Kama wewe ni mfanyabiashara iwe ya kubwa au ndogo,  kipindi hiki cha mwaka huambatana na faida lukuki za kujitangaza na kujitafutia masoko zaidi. Yafuatayo ni mambo tisa ambayo Jumia Travel inapendekeza kuwa unaweza kuyatumia kama fursa ili kuwavutia wateja zaidi na kujitangaza katika msimu huu.   

Punguzo la bei. Kwa kawaida kipindi kama hiki cha msimu wa sikukuu wateja wengi hutegemea punguzo la bei kwenye bidhaa na huduma tofauti. Unaweza kuitumia fursa hii kwa kutoa punguzo la bei pia. Mbali na kutoa punguzo kwenye biashara yako lakini pia unaweza kushirikiana na wafanyabiashara wengine. Kwa mfano, kama unauza nguo unaweza kutoa punguzo la bei ambapo wateja wakifanya manunuzi ya kiwango fulani watajipatia fursa ya kupata chakula kwenye mgahawa fulani.

Maazimio ya biashara kwa mwaka ujao. Kama ni mfanyabiashara ambaye una dira na malengo ya kuifikisha biashara yako mahali fulani lazima utakuwa na maazimio. Unaweza kukitumia kipindi hiki kwa kuwajulisha wateja wako maboresho unayotarajia kuyafanya mwaka ujao ili kuwavutia zaidi.

Chakula. Hakuna mtu asiyependa chakula. Zipo njia nyingi za kuwashukuru wateja na wadau mbalimbali waliofanikisha kwa namna moja ama nyingine kufikia hapo ulipo. Unaweza ukaanda chakula cha pamoja na kupata fursa ya kuzungumza na kujadili masuala mbalimbali yanayoweza kusaidia kukua kwa biashara yako.

Kadi za kushukuru. Nguvu ya kushukuru kwa kutendewa jambo fulani ni kubwa tofauti na unavyofikiri. Kwa kuonyesha kwamba unajali na kutambua mchango wa wateja kwenye biashara yako kunaweza kufungua milango mingi zaidi. Unaweza kuandaa kadi zenye ujumbe mzuri wa shukrani na kuwatumia wateja wako njia ya barua pepe au kuwapatia pale wanapotembelea biashara yako.

Mauzo kwa wateja maalumu. Kila biashara inakuwa na wateja ambao ni waaminifu kwa namna moja ama nyingine. Kwa kutambua mchango wao unaweza kuandaa mauzo maalumu kwa ajili yao. Unaweza kulifanikisha hili kwa kuandaa kuponi na kuwapatia kisha kuwajulisha kwamba wanaweza kutembelea kwenye biashara yako na kufanya manunuzi ya kiwango ulichowapatia.
Saidia jamii inayokuzunguka. Miongoni mwa mbinu ya kujenga uhusiano mzuri na jamii inayokuzunguka na ili kukubalika ni pamoja na kutoa msaada kwa masuala mbalimbali. Zipo nyanja mbalimbali unaweza kulifanikisha hili. Fanya utafiti mdogo kujua changamoto zinazoizunguka jamii yako na kisha omba kutoa mchango wako. Inaweza kuwa ni usafi wa mazingira, elimu, watoto yatima nakadhalika.

Andaa shindano dogo kwa wateja. Kama mfanyabiashara unaweza ukaandaa shindano dogo kwa wateja wanaotembelea dukani kwako na kisha kujishindia zawadi mbalimbali. Unaweza ukaweka tangazo nje ya duka lako ambapo unaweza kuwavutia hata wapita njia.    

Andaa burudani kidogo. Haijalishi biashara yako ipo kwenye hali gani lakini unaweza ukaanda chochote kuwaburudisha wateja wako. Zipo namna nyingi za burudani kama vile kuandaa michezo kwa ajili ya watoto au hata burudani ya muziki.

Tumia mitandao ya kijamii kushirikisha matukio yote. Kwa dunia tunayoishi sasa kamwe hauwezi kuidharau nguvu ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Instagram na Youtube. Itumie fursa inayoitoa mitandao hii kuwashirikisha wateja wako na jamii kwa ujumla mambo yanayotukia kwenye biashara yako na utaona mabadiliko.

Zipo njia nyingi ambazo unaweza kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara na sehemu tofauti ili kuongeza thamani ya biashara yako. Jumia Travel inakushauri kujaribu kufanya kitu tofauti katika biashara yako kabla ya mwaka kuisha. Ubunifu ni kitu muhimu ili kukua zaidi lakini pia jifunze kutoka kwa wafanyabiashara wengine wanatumia njia zipi kufanikiwa.

WANANCHI SIMIYU WAENDELEA NA USAJILI WA VITAMBULISHO VYA TAIFA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikao 12 ya Tanzania inayoendelea na zeozi la kuwasajili wananchi kwa lengo la kuwapatia Vitambulisho vya Taifa.
Kwa sasa zoezi hilo limeingia kwenye awamu ya pili ya Usajili katika wilaya zote za mkoa huo ambazo ni Bariadi, Meatu, Busega, Maswa na Itilima huku mwitikio wa watu ukiwa mkubwa.
wanaoshiriki kwenye zoezi hilo ni wananchi wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, wageni na Wakimbizi.

Pichani ni Maafisa Usajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wakiwachukua alama za Kibaiolojia wananchi wa mkoa wa Simiyu Kijiji cha  Mwakiboro wakati zoezi la Usajili likiendelea .
Zoezi la Usajili likiendelea katika Kijiji cha Kilulu wilayani Bariadi 

Wananchi wa Kijiji cha Mwakiboro mkoani Simiyu wakisubiri kupatiwa huduma ya Uandikishwaji Vitambulisho vya Taifa.
 

BARIADI KUTUMIA BILIONI 4.9/- KUJENGA STENDI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Imeandikwa na Shushu Joel, Bariadi
HALMASHAURI ya mji wa Bariadi, Simiyu imesaini mkataba wa Sh bilioni 4.9 na kampuni ya JV Kings & Helem Contractors ya Dar es Salaam kujenga stendi ya kisasa ya mabasi Somanda na kilomita 1.5 za barabara ya lami.
Akizungumza kabla ya kusaini mkataba huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Bariadi Melkizedeck Humbe, alisema fedha za mradi huo zimetolewa kwa mkopo na Benki ya Dunia.
Alisema mradi huo utajumuisha ujenzi wa nyumba na ujenzi wa barabara hiyo kutoka Bariadi Sekondari hadi Nyamhimbi na barabara ya Ikulu kwenda ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Alisema mkataba huo utatekelezwa ndani ya mwaka mmoja na akawataka wakandarasi hao kuzingatia mikataba kuhusu suala la mazingira.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Bariadi, Robart Lweyo alisema ujenzi huo utaharakisha maendeleo kwani miundombinu ikikamilika halmashauri hiyo itapata ushuru wa mabasi.
Lweyo alimtaka mkandarasi huyo kuzingatia muda wa mkataba huo akisema baadhi ya wakandarasi wanafanya miradi mingi mwisho wake inawashinda kukamilisha kwa wakati. Mhandisi wa JV Kings & Helem Contractors, Happy Lebe alisema watajitahidi kutekeleza mradi huo kwa haraka ili ikiwezekana wakamilishe kabla ya mkataba huo kuisha.
CHANZO HABARI LEO
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Simiyu Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa